Hii sasa ishakuwa tabu! Courtois akacha mazoezi Chelsea

London, England. Kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois anayehusishwa na kutakiwa na Real Madrid, ameshindwa kuhudhulia katika mazoezi ya timu hiyo jana Jumatatu.

Taarifa zinasema Chelsea ‘Blues’ hawajui ni lini kipa huyo wa Ubelgiji mwenye miaka 26, atarejea mazoezini.

Courtois amekuwa mchezaji wa Blues tangu 2011, wakati aliposajiliwa kutoka klabu ya Ubelgiji ya Genk na baadaye alitolewa kwa mkopo Atletico Madrid.

Winga wa Chelsea, Eden Hazard naye amekuwa akihusishwa kutakiwa na Real, lakini alishiriki katika mazoezi ya Jumatatu.

Courtois alishinda tuzo ya kipa bora wa Kombe la Dunia Russia, baada ya kuiongoza Ubelgiji kuichapa England na kumaliza nafasi ya tatu.

Kipa huyo amecheza mechi 154 akiwa na Chelsea, amefanikiwa kucheza mechi 58, bila ya kufungwa huku akiruhusu mabao 152.

Kocha mpya wa Blues, Maurizio Sarri alisema hana uhakika kama Courtois atabaki katika timu hiyo.

Alisema: "Hadi sasa Courtois ni kipa wa Chelsea. Sijui nini kitatokea baadaye. Itategemea na uamuzi wa klabu, uhususani yeye mwenyewe, lakini ni matumaini yangu Courtois ataendelea kuwa kipa wetu."

Chelsea ilichapwa mabao 2-0 na Manchester City katika mchezo wa Ngao ya Jamii iliyochezwa Jumapili na goli alikuwa kipa Muargentina Willy Caballero.