Hii Harambee Stars mambo yamebana

EWE! Ni kama kuota usingizini umeabiri Ulaya wakati unamburika unajipata ungali mtaani tu. Ndo Harambee Stars, timu ya taifa inayopiga hatua moja mbele na mbili nyuma.

Juzi ililambwa mabao 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye mtanange wa pili wa kirafiki kule Morocco. Mabao ya Eric Johanna na Michael Olunga hayakuifaa Stars hata kidogo na maji yalizidi unga kipindi cha pili beki Ismael Gonzalez alipoonyeshwa kadi nyekundu kwa kutumia lugha chafu na kuwafanya vijana wa Stanley Okumbi kumaliza wakiwa kumi uwanjani.

“Kuna kazi nyingi ya kufanya kabla ya kuchuana na Ghana mwezi Septemba. Hakuna kitu kilichofanya kazi huku, tulifanya makosa mengi sana si kawaida kwa timu ya taifa,” alisema Naibu Kocha, Frank Ouna.

Na hapa ndo wadau wa soka wameelezea kutoridhika kwao na jinsi Stars inavyoendeshwa.

“Paul Put aliwakataa hawa makocha wasaidizi sasa tunajionea wenyewe alichomaanisha,” alisema shabiki Paul Mulemi.

“Tuliambiwa timu itakua na kocha kabla ya kuelekea Morocco kwa mechi za kirafiki, kwani huyo kocha atapata muda lini kufahamu wachezaji wake kama angali hajatua? aliongeza shabiki mwingine, Francis Ngira.

Stars inarejea nchini leo Alhamisi huku wachezaji wengi wanaocheza nje wakipitiliza kwenye klabu zao moja kwa moja.