Heri ya uzee wa kina Kagere kuliko ubishoo wa vijana wetu

TUNAJUA tunadanganywa sana na nyota wa kigeni wanaokuja nchini kucheza soka la kulipwa katika klabu zetu. Tunajua wengi huwa na umri mkubwa zaidi na ule uliopo kwenye pasipoti zao. Ni vigumu kuamini kirahisi, eti Meddie Kagere ana miaka 32. Akili haikubali. Sio kwa sababu ya mwonekano wake, lakini hata rekodi zake za uchezaji soka nazo zinamkana. Ni vigumu pia kuamini Emmanuel Okwi ni mdogo kwa John Bocco au utakubali vipi kirahisi eti, Amissi Tambwe anajiandaa kutimiza miaka 29?

Udanganyifu huu wa umri haupo kwa wageni tu, hata baadhi ya nyota wetu wanatupiga fiksi sana kwa kujifanya viserengeti boys, ilihali ni vibabu. Wengi wanaotudanganya tunawajua!

Bahati mbaya kasumba hii ya udanganyifu kwa nchi za Afrika, haupo kwa wanasoka tu, bali hata mastaa wa muziki, filamu na urembo wana tatizo hilo. Wanawadanganya sana mashabiki wao kwa kujifanya vitoto vidogo, ilihali wengi wao wamekula chumvi za kutosha. Wanasahau utotoni mitaani walicheza na watoto wenzao. Wameishi ndani ya jamii hivyo inayowajua kuliko wanavyojijua wenyewe.

Upo mfano halisi juu ya staa wa filamu ambaye mwaka 2003 alishiriki Miss Mabibo 2003, huku akijidai ana umri wa miaka 19. Nasema alijidai kwa vile miaka miwili nyuma alishiriki Miss Mwanza na Singida kwa kutumia umri huohuo wa miaka 19.

Katika shindano hilo la Miss Mabibo alishika nafasi ya pili kabla ya kuja kuibukia Bongo Movie na hivi karibuni alikaririwa akidai eti, mwaka huu anajiandaa kutimiza miaka 30. Kiuhalisi kimwana huyo ana miaka 38, ni bibi ila anajifanya ni msichana ila anapata tabu sana unaambiwa!

Ni bahati tu, katika fani nyingine sio rahisi kubaini udanganyifu tofauti na ilivyo kwenye soka. Katika mchezo huu hata mchezaji ajishushe umri vipi ataumbuliwa na utendaji kazi wa mwili wake uwanjani kama alivyoumbuka JJ Okocha aliyestaafu soka ikijidai ana umri wa miaka 29.

Nani hajui umri huo ndio huwa kilele cha mafanikio ya mchezaji na kwa soka alilokuwa akilipiga Okocha ni vigumu kuamini alistaafu akiwa na umri huo tena hiari bila ya kuwa majeruhi!

Kina JJ Okocha wapo wengi ndani na nje ya nchi na angalau wachezao nafasi ya ukipa, wanamudu kuedelea kucheza kuliko nafasi nyingine hasa kiungo au ushambuliaji zinazohitaji pumzi.

Lakini unaweza kusema ni afadhali kuwa na mchezaji mzee kama Meddie Kagere ama Okwi anayeitumikia nafasi yake kwa ufanisi kuliko kuwa na vijana goigoi na wasio na faida kwa timu.

Kwa jinsi wachezaji wetu vijana wanavyoshindwa kufanya kazi uwanjani, unaona ni bora wahenga kutoka nje ya nchi waendelee kuja kutudanganya tu.

Iangalie kazi anayoifanya Kagere ama Okwi, kisha linganisha na ile ya kina Ibrahim Ajibu, Juma Mahadhi, Said Ndemla, Geofrey Mwashiuya na wengine ndio utajua namaanisha nini?

Kwa nini kina Tambwe, Kagera, Okwi, Donald Ngoma au Bruce Kangwa wasiendelee kula mishahara minono nchini iwapo kila uchao wanajua kuwapa raha mashabiki wa klabu zao?

Ulikiangalia kikosi cha Yanga kilichocheza wiki hii pale Nairobi dhidi ya Gor Mahia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kucharazwa mabao 4-0 ugenini?

Asilimia kubwa kiliundwa na vijana wenye damu inayochemka, ila uliona walichokuwa wakikifanya Uwanja wa Moi Kasarani? Kwa nini tusiendelee kuwapokea kina Kagere ili wazibebe timu zetu kwenye mechi kubwa kama hizo? Unakuwaje na straika kijana asiyeweza hata kukimbia na mpira mita tano ama kupiga shuti lolote langoni mwa adui kwa dakika zote 90? Wa kazi gani!

Mashabiki wataendelea kuwakejeli kina Kagere ama Okwi kuwa ni wahenga, vibabu na wazee, lakini kiuhalisia jamaa hao ni wazee wa kazi na wana faida kuliko vijana mabishoo na mizigo!

Simba huenda ni mashahidi kwa kazi kubwa iliyofanywa na kina Okwi na Bocco msimu uliopita na uhondo walioonjeshwa kidogo na Kagere katika mechi za Kombe la Kagame 2018.

Unaweza kuishangaa Yanga kumrejesha Mrisho Ngassa au Deus Kaseke na kuamini labda ni kwa vile klabu yao ina ukata mkali, ila kiundani utabaini usajili huo ukawa na faida kubwa kuliko unavyobezwa sasa na baadhi ya watu.

Naamini kama wachezaji vijana wangekuwa wakiifanya kazi yao kwa ufanisi na kuzibeba timu, viongozi wasingepoteza muda kubeba wachezaji wakongwe. Wasingeshindana kuleta mapro wazee kutoka nje ya nchi na pengine mamilioni ya fedha wanayolipwa wageni hao wangemwagiwa wao na kuneemeka.

Nadhani imefika wakati wachezaji vijana nchini kuchangamka na kutumia vipaji vyao kuweza kujitengenezea jina na kujiuza badala ya kuendelea kulalamika kubaniwa na maproo wa kigeni.