Hekalu la Samatta linasajili Simba yote

KAMA utaamua kubisha utakuwa ni tabia yako tu, lakini straika wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, sio mtu wa mchezo mchezo kabisa. Unajua nini? Msimu uliopita Simba ilipiga kelele sana juu ya kikosi chao cha Sh1.3 bilioni, lakini sasa ukisikia habari ya mjengo wa nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania utajua kuna tofauti ya tui na maziwa, licha ya kufanana rangi.

Samatta, ambaye pia ni nahodha wa Taifa Stars, kwa sasa yuko kwenye hatua za mwisho kukamilisha mjengo wake wa maana kule Kigamboni, ambapo ukikamilika kabisa basi utakuwa ni kivutio kwa wakazi wa maeneo ya jirani kama lilivyo Daraja la Nyerere au Daraja la Juu (fly over) inayojengwa pale makutano ya Mandela na Nyerere eneo la Tazara.

Yaani halitakuwa jambo la ajabu sana kwa watu kwenda kupiga picha jirani na mjengo huo kwani, sio wa kitoto na umegharami fedha za kutosha ambazo unaweza kufanya usajili wa kikosi cha mastaa wa maana cha Simba, Yanga na Azam na chenji inabaki.

Mjengo huo wa Samatta umechukua zaidi ya miaka mitatu sasa hadi kuwa kwenye hatua za mwisho za kukamilika, ambapo aliamua kuvunja ghorofa lake la awali baada ya kubaini limejengwa chini ya viwango.

Awali, Samatta aliamua kulivunja jengo hilo la ghorofa moja ambalo lilikuwa limekamilika tayari kwa kuanza kutumika, lakini aligundua kuwa limejengwa kwa kiwango cha chini na kupata mzuka wa kulishusha na kuweka kitu kingine.

Kwa mujibu wa baba mzazi wa Samata, Mzee Ally Samatta, jengo hilo la awali liligharimu kiasi cha Sh 500 milioni na straika huyo hakuona shida kufanya maamuzi ya kulivunja na kuanza upya ujenzi huo.

Jengo hilo la awali lilivunjwa mwaka 2016 muda mfupi baada ya Samatta kubeba tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, na kuanza kujenga hili la sasa ambalo liko hatua za mwisho tu.

Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalumu, Mzee Samatta alisema kuwa mjengo wa sasa mpaka hatua iliyofikia umegharimu zaidi ya Sh 1 bilioni na kwamba, gharama hiyo itaongezeka kwani kuna baadhi ya vitu bado havijakamilika ikiwemo vikorombwezo kibao tu.

Msimu uliopita wa Simba ambayo ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilifanya usajili wa maana kwa kunasa mastaa kibao, ambapo ilitumia Sh 1.3 bilioni kwenye usajili wake, lakini unaambiwa fedha alizotumia Samatta mpaka sasa nyumba yake ikiwa inaelekea kukamilika ni zaidi ya fedha zilizotumiwa na Simba kwenye usajili wao uliopita.

Kwa kutumia pesa hiyo, Simba ndio timu iliyotumia pesa nyingi kwenye usajili kwa timu za Tanzania na huenda ikawa imeongoza kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutumia pesa za maana kwa kusajili wachezaji nyota.

“Nafurahi sana kuona akili ya mwanangu inaendana na mimi kwani nilikuwa napenda sana kuwekeza kwenye ardhi, ametumia akili sana kuwekeza tofauti na watu wengine ingawa wachezaji wengi wa Afrika siku hizi wana akili kama Samatta kuwekeza kwenye ardhi.

“Hii nyumba imetumia pesa nyingi sana, mpaka sasa inafika Sh 1 bilioni ingawa hadi kukamilika kwake zitakuwa zimeongezeka na hapa bado nyumba haijamalizika kama anavyotaka mwenyewe, “ alisema Mzee Samatta

Mwanaspoti lilifika kwenye mjengo huo uliopo eneo la Kibada likiwa sambamba na Mzee Ally Samatta, ambaye alieleza mambo kibao kuhusiana na mjengo huo na Samatta mwenyewe.

Kuanzia kesho Jumatatu, Mwanaspoti kama kawaida yake litaanza kuchapisha mfululizo wa makala ikieleza hatua kwa hatua juu ya hekalu hilo. Kiwanja kilipatikana vipi, vikwazo kabla ya ujenzi na majirani je. Vipi kuhusu Samatta kuficha siri. Hakikisha unapata nakala yako.