Heh! Amissi Tambwe anamdai Okwi

Muktasari:

  • Wadau wa soka nchini wanamtazama Okwi kama shujaa wa msimu huu. Matarajio yamekuwa makubwa kwake. Hata hivyo, Okwi ana kazi kubwa ya kuvunja rekodi ya mkali wa mabao Ligi Kuu Bara, Amissi Tambwe.

EMMANUEL Okwi ndiyo habari ya mjini kwa sasa. Amefunga mabao sita katika dakika 180 alizocheza kabla ya mchezo wa jana Alhamisi dhidi ya Mbao FC. Ni rekodi ya maana.

Wadau wa soka nchini wanamtazama Okwi kama shujaa wa msimu huu. Matarajio yamekuwa makubwa kwake. Hata hivyo, Okwi ana kazi kubwa ya kuvunja rekodi ya mkali wa mabao Ligi Kuu Bara, Amissi Tambwe.

Tathmini inaonyesha kuwa Tambwe ambaye alitua nchini kwa mara ya kwanza Julai 2013, ana rekodi za kusisimua ambazo huenda zikampa wakati mgumu Okwi kuzivunja.

Angalia hii;

Mabao 21

Tambwe ndiye straika wa kizazi kipya aliyeweza kufunga mabao mengi kwenye msimu mmoja. Miaka ya nyuma, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliwahi kufunga mabao 26 kwa msimu mmoja. Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar aliwahi kufunga 25 kwa msimu mmoja.

Lakini kwa kizazi cha sasa, Tambwe ndiye aliyefunga mabao 21. Wengine wote wamefunga chini ya hapo. Tambwe alifunga mabao hayo msimu wa 2015/16 na kuwa mshambuliaji wa sasa aliyefunga zaidi.

Okwi atahitaji kufunga mabao 15 ama zaidi kwenye mechi zilizosalia ili kuifikia rekodi hiyo.

HAT TRICK SITA

Hapa kazi ipo. Tambwe ana rekodi ya kufunga hat trick sita katika misimu yake minne aliyocheza hapa nchini. Alifunga mbili kwa misimu mitatu mfululizo. Okwi tangu ameanza kucheza nchini ndiyo kwanza ana hat trick mbili tu. Atazifikia sita za Tambwe?

MABAO MECHI MOJA

Okwi tayari amemlipa Tambwe rekodi yake ya kufunga mabao manne kwenye mchezo mmoja lakini bado ana deni. Tambwe alifunga mabao manne dhidi ya Mgambo JKT mwaka 2013 lakini alirudia tena dhidi ya Coastal Union mwaka 2015 wakati Yanga ikishinda 8-0.

Okwi tayari amefunga mabao manne dhidi ya Ruvu Shooting wakati Simba 7-0, lakini atahitaji kufunga tena ili kumlipa Tambwe.

UFUNGAJI BORA

Okwi tangu aanze kucheza nchini hajawahi kuwa Mfungaji Bora, labda itokee msimu huu. Tambwe tayari ametwaa tuzo hiyo mara mbili, mwaka 2014 na 2016. Okwi ana deni kubwa la kufikia rekodi hiyo. Anatakiwa kufunga mabao mengi angalau atwae tuzo hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu hasa nyakati hizi ambazo Tambwe anasumbuliwa na majeraha.

MECHI YA WATANI

Okwi na Tambwe wana rekodi moja inayofanana. Kila mmoja amefunga mabao matatu katika mechi zilizozihusisha Simba na Yanga. Okwi ameifunga Yanga mabao matatu sawa na Tambwe aliyoifunga Simba. Tofauti iko wapi? Tofauti ni kwamba Tambwe alifunga mabao yake kwenye mechi tatu mfululizo dhidi ya Simba wakati Okwi alifunga mawili mwaka 2012 na jingine moja 2015.

HAT TRICK FA

Okwi hajawahi kushiriki Kombe la FA na mwaka huu itakuwa mara yake ya kwanza lakini Tambwe aliwahi kufunga hat-trick kwenye FA dhidi ya Ashanti wakati Yanga iliposhinda 4-1. Wengine ni Atupele Green na Obrey Chirwa.