Hazard ajitangazia dau lake

Muktasari:

Kiungo Mbelgiji amekuwa akihusishwa na kutakiwa na Real Madrid mara kwa mara

LONDON, ENGLAND. Kiungo wa Chelsea, Eden Hazard ameweka wazi dau lake kuwa ni Euro 350 milioni kwa anayetaka kumsajili.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ubelgiji anaamini yeye ndiye mchezaji mwenye ubora na thamani ya kuvunja rekodi ya dunia ya uhamisho inayoshikiliwa na Mbrazili, Neymar kwa sasa.

Neymar alihama kutoka Barcelona kwenda Paris Saint-Germain kwa ada ya Euro 222 milioni kwenye dirisha lililopita.

Akizungumzia thamani yake, Hazard alisema: "Itakuwa jambo muhimu sana kama Chelsea itaweka kiwango cha pesa kwa timu itakayohitaji kunisajili. Ndiyo hivyo, soka lilivyo.

“Tangu Neymar aliposaini kwa pesa nyingi hivyo, nadhani kwa sasa kila mchezaji wa kiwango kama chake anapaswa kununuliwa kwa pesa nyingi.

"Hakuna tatizo, mimi ninachowaaambia kwa sababu, nitajaribu kucheza kwa kiwango changu bora. Mkataba wangu umebaki miaka miwili na tutaona kitakachotokea. “Niliwaambia thamani yangu ilikuwa Euro 300 milioni, miezi miwili hii nimeongeza Euro 50 milioni, hivyo nina thamani ya Euro 350 milioni."

Hazard anatamba hivyo huku kikosi chake cha Chelsea leo Jumamosi kikiwa ugenini kwa West Ham United kupambana na hali yao katika kujaribu kupunguza pengo la pointi baina yao dhidi ya Manchester City inayoshikilia usukani. Chelsea ipo nafasi ya tatu na pointi zake 32, pointi 11 nyuma ya vinara Chelsea.