Hazard: Mourinho alimpoteza Salah

Muktasari:

Winga huyo wa Misri alishindwa kutamba Chelsea chini ya kocha Mreno huyo

London,England. Edin Hazard amedai Jose Mourinho alikuwa kikwazo kwa kiungo wa pembeni wa Liverpool, Mohamed Salah.

Hazard alisema Mourinho alimnyima fursa mchezaji huyo kuonyesha ubora wake alipokuwa kocha wa Chelsea alipodumu kwa miezi 12.

Mourinho aliwahi kumfundisha Salah kabla ya kupelekwa kwa mkopo Fiorentina mwaka 2015 na msimu uliopita majira ya kiangazi alitua Liverpool.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji alisema Mourinho hakumtendea haki Salah licha ya kuwa mchezaji mwenye kiwango bora.

“Hakupata nafasi ya kuonyesha kiwango labla kwasababu ya kocha au wachezaji, lakini alipaswa kubaki hapa muda mrefu,” alisema Hazard.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri alitua  Liverpool kwa Pauni 12 milioni na amekuwa akicheza kikosi cha kwanza chini ya kocha Jurgen Klopp.

Hazard alisema Chelsea ilifanya kosa kumpiga bei mchezaji huyo kwa kuwa alikuwa hazina Stamford Bridge.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 25, amefunga mabao 14 katika michuano mbalimbali msimu huu na wachambuzi wa soka wanamtabiria mafanikio Anfield.