Hawafanyi mazoezi, ila ukiwapa mpira utapenda

Muktasari:

  • Kocha Emery anaripotiwa kuwa na mazoezi magumu sana, lakini Wenger anachodai ni kwamba staa huyo si mchezaji wa kufanyishwa mazoezi, hahitaji hilo kucheza vizuri ndani ya uwanja. Usimfanyishe mazoezi Ozil, kisha mwingine uwanjani, atakupa matokeo.

UNAI Emery kwa sasa anaripotiwa kuwa na shida juu ya kumtumia supastaa wa Kijerumani, Mesut Ozil. Pengine, Emery anahitaji kumpigia simu Arsene Wenger na kumuuliza namna nzuri ya kumtumia fundi huyo wa mpira ili akuletee matokeo mazuri uwanjani.

Kocha Emery anaripotiwa kuwa na mazoezi magumu sana, lakini Wenger anachodai ni kwamba staa huyo si mchezaji wa kufanyishwa mazoezi, hahitaji hilo kucheza vizuri ndani ya uwanja. Usimfanyishe mazoezi Ozil, kisha mwingine uwanjani, atakupa matokeo.

Hii ndio orodha ya wachezaji ambao hawapendi kufanya mazoezi, lakini ukiwapa nafasi ya kucheza uwanjani, watakupatia matokeo matamu.

5.Mesut Ozil

Januari 2016, akiwa kwenye kiwango matata kabisa, Mjerumani Mesut Ozil alikuwa na maisha ya raha sana huko Arsenal. Chini ya Arsene Wenger, Ozil hakuhitaji sana kufanya mazoezi. Yeye alichokuwa akihitaji kumpanga tu kwenye mechi, atakufanyia kile unachotaka akifanye mchezoni.

Wenger alisema siri kubwa aliyokuwa akifanya kumfanya Ozil kuwa bora uwanjani ni hivi: “Mesut, nilimpa mapumziko ya wiki moja baada ya mechi za kimataifa. Hakuwa akifanya mazoezi, nilikuwa nampumzisha siku zile za mechi. Ni mchezaji ambaye anahitaji kuwa na uhuru wa kumpimzika kabla ya mechi, kisha nenda kampanga uwanjani, utaona atakachokupatia.”

4.George Best

Kuhusu Best kufanya mazoezi hilo ni jambo ambalo lilifahamika wazi, hapendi. Januari 1972 alikosekana wiki nzima mazoezini huko Manchester United na badala yake alikuwa akiponda raha na Miss Great Britain. Alikuwa ni mchezaji ambaye hakuhitaji kufanya mazoezi kuonyesha uwezo wake wa kuucheza mpira. Alikuwa mchezaji ambaye atakukasirisha kwa kukosa mazoezi kwa muda mrefu, lakini akija kwenye mechi moja tu anafunga mabao sita na kukufanya uwe na furaha, usikumbuke tena kama hakuwapo mazoezini wiki nzima.

3.Ronaldo

Ni mmoja wa wachezaji bora kabisa waliopata kutokea duniani. Lakini, kama hukuwa unafahamu, Ronaldo hakuwa anapenda kabisa kufanya mazoezi. Kocha wake, aliyekuwa akimtoa huko Inter Milan, Gigi Simoni, alilitambua hilo na kusema kwamba hakuwa akimtaka mchezaji huyo afanye mazoezi wanayofanya wenzake na alisema: “Sidhani kama wachezaji wote wanapaswa kunolewa kwa staili moja, hasa kwa wale spesho. Ronaldo alikuwa mmoja wao.

“Sijawahi kumwambia Ronaldo akimbie mazoezini, nilimtaka afanye mazoezi ya kuuchezea mpira tu, waache wengine huko wakimbie kwa ajili yake.”

Fabio Capello alipomnoa Ronaldo huko Real Madrid mwaka 2006, likumbana na mchezaji huyo akiwa ameongezeka uzito na kumtaka apungua, kitu ambacho hakikufanikiwa. Lakini, bado Capello hadi sasa anamtaja Ronaldo kama ni mchezaji bora zaidi aliyewahi kumnoa.

2.Romario

Romario ni mchezaji mwingine ambaye hakuwa akifanya mazoezi kabisa. Kipaji chake cha soka kiliwafanya hata makocha kutohangaika nao kuwafanyisha mazoezi. Mfano mzuri ni mwaka 1994 tu hapo, Johan Cruyff si kwamba alimruhusu Romario kukosa mazoezi, bali alimtoa uwanjani mapema ili awahi tamasha huko Rio De Janeiro.

“Kuna wakati, Romario aliniomba kama anaweza kukosa mazoezi kwa siku mbili ili arudi kwao Brazil kwenye tamasha,” alisema Cruyff. “Nilimjibu: ‘kama utafunga mabao mawili kesho, nitakuwa siku mbili za ziada za mapumziko kuliko wengine.’ Siku iliyofuata, Romaria akafunga bao lake la pili dakika ya 20 tu na hapo akanipa ishara ya kumruhusu aondoke. Akaja kuniambia: ‘Kocha, ndege yangu inaondoka saa moja lijalo.’”

1.Ronaldinho

Hebu msikie mchezaji aliyewahi kucheza na Ronaldinho huko PSG, Jerome Leroy, akisema: “Ronaldinho hakuwa akifanya mazoezi siku yoyote ile ya wiki. Alikuwa akionekana Ijumaa ambayo kesho yake Jumamosi kunakuwa na mechi.

“Huyo alikuwa Ronaldinho. Nadhani alikuwa akifuata nyayo Romario, ambaye alikuwa na mitoko mingi usiku. Na hiyo asubuhi yenyewe aliyokuwa akija mazoezini, utamwona tu amevaa miwani yake na kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha kufanyia masaji anaenda kulala. Wachezaji wenye vipaji vilivyopitiliza wakati mwingine wanakuwa kama wajinga hivi.”