Hawa wakitua tu Simba mmekwisha

Muktasari:

  • Nilipiga naye stori tena akasisitiza kusema, amekitazama kikosi chake, amefanya tathmini akaja na majawabu ya kuifumua Simba na baadhi ya wachezaji atawapa mkono wa kwaheri.

KOCHA Mfaransa wa Simba, Pierre Lechantre hatanii, nilipiga naye stori kuhusu timu yake kabla ya mchezo, akasema atafanya kitu.

Nilipiga naye stori tena akasisitiza kusema, amekitazama kikosi chake, amefanya tathmini akaja na majawabu ya kuifumua Simba na baadhi ya wachezaji atawapa mkono wa kwaheri.

Kocha huyo ambaye timu yake imetolewa kwenye Kombe la Shirikisho na Al Masry juzi usiku, alisisitiza msimu huu ukimalizika tu, lazima akifumue kikosi na kuvuta nyota wapya sita kwa mpigo ili kukifanya kitikise michuano ya kimataifa.

Lechantre anaonekana kuna kitu anaona kinamisi Simba, akasema anaona wachezaji kama John Bocco na Emmanuel Okwi, lakini tatizo ni kwamba kuna wengine ni kama mizigo kwa kushindwa kuisaidia timu hiyo.

Mfaransa huyo aliyewahi kuzinoa kwa mafanikio timu za taifa za Cameroon na DR Congo alisema kwa hali ilivyo anahitaji nyota wapya sita watakaoweza kuibadilisha timu na kuifanya iwe na makali ndani na nje ya nchi na si kuangalia Ligi Kuu pekee.

Alisema pamoja na maeneo mengine, watalazimika kuboresha safu yao ya kiungo pamoja na washambuliaji.

“Kwa ujumla tunahitaji wachezaji wenye uwezo wa kucheza mechi za ndani na hizi za kimataifa. Tukikosa kwenye Ligi ya ndani tutalazimika kutafuta wa kutoka nje,” alisisitiza.

Alisema Bocco na Okwi ambao wamefunga mabao 34 kwenye mashindano yote msimu huu, wanaitendea haki nafasi hiyo lakini tatizo ni kwamba hawana mbadala, endapo wawili hao wakikosekana kwa pamoja.

“Ukiwakosa Bocco na Okwi unachanganyikiwa, ukitazama kwenye timu hakuna mchezaji mwingine wa kukubeba. Hawa ni wachezaji hatari si tu hapa Tanzania, bali Afrika.

“Tunahitaji kuwa na wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa kama wao au zaidi. Mavugo (Laudit) ni mzuri lakini tulipofika hapa hakuwa fiti hata kidogo, walau sasa tunamsaidia,” alisema Lechantre.

Kwa upande wa kiungo alisema waliopo sasa wengi sasa wengi ni washambuliaji hivyo wanahitaji kupata viungo wengine wa kusaidia kukaba.

“Tunahitaji pia wachezaji wa kukaba zaidi. Tuna viungo wengi wazuri lakini kwenye kushambulia. Wengi wakipoteza mpira hawasaidii sana kwenye kukaba, hiyo ndiyo sababu wakati mwingine tunalazimika kumtoa James Kotei kwenye beki na kumpanga kiungo,” alisema Lechantre.

Katika upande mwingine, Lechantre alisema kuna baadhi ya wachezaji ambao timu hiyo italazimika kuachana nao mwishoni mwa msimu kwa kuwa hawana uwezo wa kuitumikia timu hiyo.

“Kuna wachezaji hapa wana uwezo wa kawaida, unashangaa imekuwaje wako Simba. Si kwamba hawajitumi, hapana, ila sio wa daraja la Simba, Simba ni timu kubwa,” alisema.

REKODI YA MAANA

Simba imetolewa Kombe la Shirikisho na Al Masry ya mjini hapa kwa faida ya bao la ugenini baada ya mchezo wa marudiano kumalizika kwa suluhu lakini habari kubwa ni kwamba mabingwa hao wa zamani wameacha rekodi ya maana.

Rekodi zinaonyesha haijawahi kutokea Simba ikacheza mechi mbili dhidi ya timu yoyote ya hapa Misri bila kupoteza mchezo hata mmoja hivyo matokeo dhidi ya Al Masry yameweka rekodi mpya Msimbazi.

Kipindi cha nyuma Simba iliwahi kucheza na timu za Ismailia, Al Ahly na Zamalek za hapa Misri na licha ya kupata ushindi jijin Dar es Salaam, ilipokuja nchini humu ilipokea kipigo.

Rekodi kubwa waliyokua nayo Simba ni ya kuwaondosha Zamalek kwa mikwaju ya penalti baada ya wao kushinda 1-0 jijini Dar es Salaam na kisha kupoteza kwa idadi kama hiyo kwenye mechi ya marudiano mjini Cairo.

Simba pia haijawahi kupata angalau sare ugenini dhidi ya timu kutoka Algeria, Morocco na Tunisia ambazo pia zinatoka ukanda huu wa Afrika Kaskazini hivyo matokeo dhidi ya Al Masry yameiweka juu na kuthibitisha Simba ya sasa sio ya mchezo mchezo.

Awali ilicheza na Es Setif, Raja Casablanca na Haras El Hadood kutoka kwenye nchi hizo lakini ilipoteza mechi zote za ugenini.

Lechantre alisema kwa namna timu yake ilivyocheza kwa nidhamu kubwa, kama angekuwa na wachezaji wawili ama watatu wenye uzoefu mkubwa basi wangewang’oa Waarabu hao.

“Tulipangilia mchezo vizuri na tulifanikiwa kwa kiwango kikubwa. Dakika 60 za mwanzo tulikaba na baadaye tukafunguka na kushambulia. Unaweza kuona Al Masry waliomba mpira umalizike, wakaamua kujiangusha ovyo.”