Hawa ndio watabeba mikoba ya Koeman

Muktasari:

Ni kocha ambaye hakika Everton na mashabiki wake wote watakuwa kwenye furaha kubwa kama wataipata huduma yake huko Goodison Park

LIVERPOOL, ENGLAND. RONALD Koeman si kocha wa Everton, ameshafutwa kazi. Kipigo kizito cha mabao matano kutoka kwa Arsenal juzi Jumapili kimehitimisha miezi 16 ya Mdachi huyo kuendelea kuwapo Goodison Park na hii hapa ndiyo orodha ya makocha wanaopatikana sokoni kwa sasa wanaoweza kurithi nafasi yake.

Carlo Ancelotti

Ni kocha ambaye hakika Everton na mashabiki wake wote watakuwa kwenye furaha kubwa kama wataipata huduma yake huko Goodison Park. Lakini, shida iliyopo ni kwamba hakuonekani kuwapo na uwezekano huo.

Ancelotti kwa sasa hana kazi baada ya kufukuzwa Bayern Munich na mwenyewe alisema anahitaji mapumziko kidogo kabla ya kurejea kwenye soka mwakani, hivyo kuna kazi kubwa ya kumbadili mawazo yake.

Luis Enrique

Kocha wa zamani wa Barcelona na AS Roma hana kazi tangu alipoachana na wababe wa Nou Camp mwishoni mwa msimu uliopita. Enrique, ambaye amewahi kulibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ni mmoja kati ya makocha wenye uwezo mkubwa na hakika atakuwa mtu muhimu kama.

Chris Coleman

Hakuna kitu kitakachomfanya Coleman apoteza kibarua chake huko kwenye kikosi cha Wales hasa baada ya kuifikisha nusu fainali ya Euro 2016. Wales ilishindwa kidogo tu kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia 2018 na mastaa wa timu hiyo akiwamo Gareth Bale wamekuwa wakipiga kampeni kocha huyo asiondoke. Lakini, kama Everton itakwenda na ofa nzuri inaweza kumnasa na kwenda kuinoa timu yao ambayo kwa sasa ipo kwenye matatizo makubwa kwenye Ligi Kuu England na Europa League.

Laurent Blanc

Hajahusishwa na kibarua chochote kwa siku za karibuni, lakini kocha huyo wa zamani wa PSG anaweza kushawishika na kurudi kwenye ukocha kama kutakuwa na ofa nzuri mezani.

Blanc amepata uzoefu baada ya kuinoa PSG na kubeba mataji ya Ligi ya Ufransa mara tatu huku akiwa na uzoefu wa soka la kimataifa baada ya kuwahi kufanya kazi kwenye kikosi cha Les Bleus.

Mchakamchaka wa Ligi Kuu England anaufahamu kutokana na kuwahi kucheza kwenye kikosi cha Manchester United, hivyo atakuwa na maarifa ya kushinda mechi za kwenye ligi hiyo.

David Moyes

Ripoti zilizoibuka hivi karibuni ni kwamba, Everton inafikiria mpango wa kumrudisha kocha wake wa zamani, David Moyes. Everton inamfikiria Moyes baada ya kuchoshwa na Ronald Koeman, kocha ambaye kwenye dirisha lililopita ilimpatia kila kitu kwa kumsajili wachezaji aliowataka ili timu ifanye vizuri.

Everton ilitumia zaidi ya Pauni 150 milioni kusajili, lakini matokeo yake kwenye ligi ni mabovu kwelikweli ikiwa imeshinda mechi mbili tu, sare mbili na vichapo vitano katika mechi tisa ilizocheza.