Hawa ndio wasimamizi halali wa mali zote za klabu

Muktasari:

Hata hivyo, tunaangalia kuhusu nidhamu na hatua zitakazochukuliwa bodi hiyo kwa mwanachama au kiongozi atakayekwenda kinyume.

Katika mwendelezo wa makala haya ya Katiba Mpya ya Simba, jana Jumamosi tuliona namna Bodi ya Wakurugenzi inavyofanya kazi kutokana na jinsi muundo ulivyo.

Hata hivyo, tunaangalia kuhusu nidhamu na hatua zitakazochukuliwa bodi hiyo kwa mwanachama au kiongozi atakayekwenda kinyume.

Ibara ya 34: Hatua za Kinidhamu

1. Onyo

2. Karipio

3. Kurudisha tuzo

4. Kusimamishwa

5. Kufukuzwa

6. Bodi ya Wakurugenzi itaandaa kanuni za nidhamu na za maadili pasipokuwa na kanuni za nidhamu na za maadili za Simba Sports Club Company Limited, Kanuni za nidhamu na za maadili za TFF au FIFA zitatumika.

Ibara ya 35: Kamati ya Nidhamu

1. Simba Sports Club inatambua Kamati ya Nidhamu ya Simba Sports Club Company Limited, itakayokuwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watatu watakaoteuliwa na bodi ya wakurugenzi, mwenyekiti na makamu mwenyekiti lazima wawe na taaluma ya sheria.

2. Chombo hiki kitasimamia Katiba ya Simba Sports Club kwa kutumia kanuni zake za nidhamu au kanuni za TFF iwapo kanuni za nidhamu za Simba Sports Club Company Limited hazipo.

3. Kamati itapitisha uamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmojawapo akiwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti.

4. Kamati inaweza kutangaza hatua za kinidhamu zilivyoelezwa katika katiba hii au kanuni zilizotayarishwa kutokana na katiba hii dhidi ya wanachama, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 26(8) au wafanyakazi wa Simba Sports Club.

5. Rufaa yoyote dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya Simba Sports Club Company Limited, itapelekwa kwa kamati ya rufaa ya nidhamu ya TFF. Rufaa dhidi ya maamuzi ya TFF yanaweza pia kukatiwa rufaa CAS ambayo itakuwa na maamuzi ya mwisho.

Ibara ya 36: Kamati ya Maadili

1. Simba Sports Club inatambua Kamati ya Maadili ya Simba Sports Club Company Limited, itakayokuwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watatu watakaoteuliwa na Bodi ya Maadili lazima wawe na taalumu ya sheria.

2. Chombo hiki kitasimamia Katiba ya Simba Sports Club kwa kutumia Kanuni zake za Maadili au Kanuni za TFF, iwapo kanuni za Maadili za Simba Sports Club Company Limited hazipo.

3. Kamati itapitisha uamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmojawapo akiwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti.

4. Kamati inaweza kutangaza hatua za kimaadili zilivyoelezwa katika katiba hii au kanuni zilizotayarishwa kutokana na katiba hii dhidi ya wanachama, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 26 (8) au wafanyakazi wa Simba Sports Cluba.

5. Rufaa yoyote dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Simba Sports Cluba Company Limited itapelekwa kwa kamati ya rufaa ya maadili ya TFF. Rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Rufaa ya Maadili ya TFF yanaweza pia kukatiwa rufaa CAS ambayo itakuwa na maamuzi ya mwisho.

E. KAMATI YA UCHAGUZI

Ibara ya 37: Uanzishaji, Kazi na Majukumu

1. Kutakuwa na Kamati ya Uchaguzi wa Simba Sports Club itakayoteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo itahusika na kuandaa na kusimamia uchaguzi wa Simba Sports Club, itashauri bodi ya wakurugenzi kuhusiana na kanuni za uchaguzi. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club itafanya kazi chini ya usimamizi na maelekezo ya Kamati ya uchaguzi ya TFF.

2. Kamati ya uchaguzi itaundwa na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watatu. Mwenyekiti na makamu wa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi lazima wawe na taaluma ya sheria.

3. Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club itatekeleza majukumu yake kwa kutumia kanuni za uchaguzi za Simba Sports Club na kama hazipo kanuni za uchaguzi za TFF zitatumika.

4. Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club itapitisha maamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmoja wao akiwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti.

5. Maamuzi ya Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club yanaweza kukatiwa rufaa kwa kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF ambayo maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.

F. BARAZA LA WADHAMINI

Ibara ya 38: Muundo wa mamlaka

1. Simba Sports Club itakuwa na Baraza la Wadhamini litakalokuwa na wajumbe wanne na ndiyo watakuwa wasimamizi na wadhibiti wa mali zote za klabu zinazohamishika na zisizohamishika na watunzaji wa ‘lakiri’ (seal) ya klabu.

2. Wajumbe wa Baraza la Wadhamini watateuliwa na bodi ya wakurugenzi na kuthibitishwa na mkutano mkuu na kuanza kazi mara watakaposajiliwa, na Kabidhi Wasihi mkuu wa Serikali. Mkutano mkuu ndio utakuwa na mamlaka ya kumwondoa mjumbe/wajumbe wa Baraza la Wadhamini kutoka kwenye wadhifa huo baada ya kupata taarifa kutoka bodi ya wakurugenzi.

3. Wajumbe wa Baraza la Wadhamini ndio watakuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba Sports Club Holding Company Limited.

4. Baraza la Wadhamini litamiliki 99% ya hisa za Simba Sports Club Holding Company Limited kwa niaba ya Simba Sports Club na Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini atamiliki 1% ya hisa za Simba Sports Club Holding Company Limited kwa niaba ya Simba Sports Club.

Je unafahamu kuwa kuna ukomo wa wadhamini kwa mujibu wa Katiba hii? Fuatilia zaidi kesho Jumatatu.