Hawa ndio waliovuta mkwanja mrefu Simba

Muktasari:

Kikosi cha Simba kinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh 1.3 bilioni ambazo walitumia kufanya usajili. Bila kumsahau Asante Kwasi, ambaye analinaswa kwenye dirisha dogo, naye atakuwa ameongeza thamani zaidi.

SIMBA wamestahili kuchukua ubingwa msimu huu. Hakuna anayebisha hilo kabisa. Kikosi cha Simba ndio ghali zaidi katika Ligi Kuu Bara kuliko timu zote msimu huu. Kama haitoshi pia, kuna wachezaji wenye viwango vya juu na wazoefu.

Kikosi cha Simba kinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh 1.3 bilioni ambazo walitumia kufanya usajili. Bila kumsahau Asante Kwasi, ambaye analinaswa kwenye dirisha dogo, naye atakuwa ameongeza thamani zaidi.

Achana na mkwanja huo wa usajili, iko hivi. Katika kila mechi ambayo Simba wameshinda ama kutoruhusu kupoteza pointi kila mchezaji aliyeanza kwenye kikosi cha kwanza anapata Sh 300,000, wachezaji wa akiba Sh 200,000 na wale ambao hajavaa hata jezi waliambulia Sh 150,000.

Mwanaspoti imeangazia wachezaji 10 wa Simba ambao wamevuna mkwanja wa maana kupitia posho hizo katika kila mechi ukiwemo mbali kabisa mishahara na posho zingine ambazo hazihusiani na mechi.

Aishi Manula

Ndio mchezaji aliyevuta mkwanja mrefu zaidi kutokana kuanza katika mechi mechi zote 28 ambazo Simba wamecheza msimu huu na utamu zaidi zote alikuwa akianza.

Thamani ya posho ambayo Manula amepata msimu huu ni Sh 11.2 milioni na kushika nafasi ya kwanza kwa kukusanya pesa ndefu klabuni hapo.

Shiza Kichuya

Ameanza katika mechi 27 na posho ambayo amebunya katika mechi hizo ni Sh 10.8 milioni hapo hujajumlisha Sh 200,000 ambayo iliipata kama mchezaji wa akiba katika mechi dhidi ya Singida United pale Namfua na Simba kushinda bao 1-0, lililofungwa na Shomary Kapombe.

Jumla ya posho yake kwa msimu huu Sh 11 milioni na kushika nafasi ya pili kwa nyota wa Simba waliovuta mkwanja mwingi nje ya mshahara.

Erasto Nyoni

Mpaka sasa mashabiki wa Yanga hawataki kumsikia kabisa, anaitwa Erasto Nyoni, kiraka matata kabisa kwenye kikosi cha Simba. Msimu huu amecheza mechi 26 na amevuna Sh 8.1 milioni kama posho ya mechi.

Nyoni, ambaye amekuwa na msimu bora ndani ya Simba, alikuwa benchi kwenye mechi moja na nyingine hakuwepo kabisa, ambazo pia amevuta posho kama kawa.

John bocco

Nahodha wenyewe ambaye Simba wataendelea kumkumbuka kutokana na huduma yake bora msimu huu, licha ya kuanza akiwa mgonjwa lakini ameanza katika mechi 23 na thamani ya posho zote alizovuna zinafikia Sh 7.6 milioni.

Kwa msimu huu, Bocco alikosa mechi za Ruvu Shooting, Njombe Mji, Yanga, Mbao FC na Ndanda kutokana na kuwa majeruhi.

James Kotei

Mghana James Kotei alisimama kwenye dimba la kati akisaidia kuzuia mashambulizi kabla ya washambuliaji wa timu pinzani kuwafikia mabeki wa kati. Huduma yake msimu huu imekuwa kivutio kikubwa. Ameanza kwenye mechi 22 na hata posho yake sio ya kitoto kabisa unaambiwa.

Ameanza akitokea benchi kwenye mechi nne msimu huu, ambapo posho yake aliyovuta ni Sh 7.7 milioni mpaka sasa.

Emmanuel Okwi

Huyu jamaa ukiacha posho hizo kuna zingine kibao zinamsubiri mwanangu. Ndiye Mfungaji Bora wa VPL, lakini pia ameanza katika 22 mpaka sasa. Alitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Singida United ya mzunguko wa kwanza na hakuwepo kabisa katika mechi nne kutokana na kuwa majeruhi. Okwi amevuna Sh 7.4 milioni.

Jonas Mkude

Ameanza katika mechi 19 ambazo thamani ya posho katika mechi hizo ni Sh 5.7 milioni. Alikuwa katika wachezaji wa akiba mechi nne ambazo alipata Sh 800,000 na hakuwepo mechi nne sawa Sh 600,000. Jumla ya posho ambayo imevuta mpaka sasa Sh 7.1

Yusuph Mlipili

Ameanza katika mechi 16 msimu ambazo thamani yake inafikia Sh 4.8 milioni. Alikuwa katika benchi la wachezaji wa akiba mechi nne ambazo zimemwezesha kuvuna Sh 800,000 na hakuwepo katika mechi saba. Jumla Mlipili amevuna Sh 6.65 milioni.

Mzamiru Yassin

Kiungo huyu fundi wa mpira ameanza katika mechi 15, ambazo thamani ya posho ni Sh 4.5 milioni. Hakuwepo katika mechi moja tu na alipata Sh 150,000 huku akiwa benchi kwenye mechi 12 hivyo, kuvuna posho ya Sh 7.5 milioni

Amepata pesa nyingi kuliko Mlipili kwa sababu alikuwa katika benchi la wachezaji wa akiba kuliko kukosekana kabisa.

Juuko Murshid

Beki wa nguvu wa Simba ambaye hukabidhiwa majukumu mazito, mwenyewe ameanza katika mechi 14. Ametokea benchi katika mechi nne na alikosekana kabisa kwenye mechi 10 hivyo, kuweka kibindoni posho ya Sh 6.5 milioni.

Shomary Kapombe

Huko Singida wanaifahamu vyema shughuli yake, jamaa ni mtamu kinoma uwanjani. Kapombe amekosekana kwenye mechi 12 akiwa nje ya uwanja kupatiwa matibabu. Alirudi katika mechi dhidi ya Kagera Sugar ambayo walishinda 2-0, na tangu hapo alikuwa akikipiga mwanzo mwisho. Ameanza katika mechi 14 na kuvuna posho ya Sh 4.2 milioni mpaka sasa.

Asante Kwasi

Simba walimsajili katika dirisha dogo akitokea Lipuli FC ya Iringa na hakuwa katika kikosi hiko kwenye mechi za mzunguko wa kwanza. Alikosa mechi dhidi ya Mwadui ambayo alikuwa na kadi tatu za njano na alikaa benchi katika mechi ya Singida United.

Ameanza katika mechi 14 na thamani ya posho katika mechi hizo ni Sh 4.5 milioni.