Hawa MREFA wana mzuka kinoma

Muktasari:

Tukuyu Star iliyopangwa katika kituo cha Rukwa kwenye michuano ya mabingwa wa mikoa kuanzia Mei Mosi hadi 16 mwaka huu ina kibarua cha kuhakikisha inafanya vizuri katika hatua hiyo ili kupanda daraja la pili na kurudisha heshima yake iliyowahi kupata mwaka 1986 ilipoibuka mabingwa wa Ligi Kuu.

CHAMA cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa) kimesema kwa sasa kinatupia jicho na nguvu kwa timu za Boma FC iliyopo ligi daraja la kwanza pamoja na mabingwa wa mkoa Tukuyu Star ili kuhakikisha zinafanya vizuri na kufanikiwa kupanda daraja.

Tukuyu Star iliyopangwa katika kituo cha Rukwa kwenye michuano ya mabingwa wa mikoa kuanzia Mei Mosi hadi 16 mwaka huu ina kibarua cha kuhakikisha inafanya vizuri katika hatua hiyo ili kupanda daraja la pili na kurudisha heshima yake iliyowahi kupata mwaka 1986 ilipoibuka mabingwa wa Ligi Kuu.

Katibu Msaidizi wa Mrefa, Lucas Kubaja alisema kupanda daraja kwa timu hizo ni fursa kwa Mrefa kuona mkoa unazidi kutambulika zaidi kisoka kuliko mikoa mingine pamoja na kujenga heshima.

“Mbeya tuna timu mbili za Ligi kuu, mbii za daraja la kwanza lakini tusipozipigania hizi tutakuwa tunauwa soka sisi wenyewe kwa mikono yetu na kutojituma kwetu ndiyo mdudu pekee anayeweza kutuuwa,” alisema Kubaja.

Alisema: “Ni lazima Simba, Yanga pamoja na Azam FC zirudi Mbeya mara nne kwa msimu ili kutoa fursa ya kuongeza mapato kwa Mrefa, lakini mbali na mapato vijana wetu wataonekana zaidi kupitia soka.

“Tutapambana kufa kupona kuhakikisha hizi timu hazitakuwa na vikwazo vinavyoweza kukwamisha juhudi za wachezaji ambao wanaonekana kulipenda soka na wamejitoa kwa yote.”