JICHO LA MWEWE: Hatujawahi kuwaelewa vizuri hawa kina Dilunga

HASSAN Dilunga kwa sasa ni kiungo mpya wa Simba. Alikuwa kambini Uturuki. Miaka mitatu iliyopita alikuwa mchezaji wa Yanga kisha akaonekana wa kawaida halafu akaachwa. Ni kosa ambalo Yanga walifanya na Simba pia wanafanya.

Kwa nini Dilunga amerudi tena katika timu kubwa? Kwa sababu Mtibwa walimwamini wakampa nafasi. Alicheza kila mara. Timu ilimzunguka yeye. Akikosea sawa, akipatia sawa. Walimsikiliza zaidi kuliko yeye alivyowasikiliza.

Yanga hawakumpa nafasi hiyo. Alikuwa amezungukwa na mastaa kina Haruna Niyonzima. Mashabiki hawakuwa na muda wa kumsubiri. Kocha hakuwa na muda wa kumsubiri kwa sababu alikuwa anapata presha kutoka kwa mabosi na mashabiki wake.

Kuna mchezaji unamchukua ukijua kipaji chake. Hata hivyo, anahitaji mazingira tofauti ya kulelewa na kufikia ubora wake. Wakati mwingine anachelewa kupevuka zaidi tofauti na wachezaji wengine, anahitaji muda. Tatizo soka letu sio la kulipwa na halipo katika misingi yake.

Yanga walihitaji kumvumilia Dilunga. Hawakufanya hivyo. Nusura wafanye kosa hilo kwa Simon Msuva katika siku za mwanzo za maisha yake Yanga. Bahati nzuri inaonekana kocha wa Yanga wa wakati huo alimuamini sana, pia inaonekana Msuva mwenyewe alikuwa na roho ngumu akakubali matusi ya mashabiki wa Yanga. Akainamisha kichwa chini akacheza soka. Wengine hawawezi.

Matokeo yake Yanga na Simba zimeendelea kupoteza wachezaji wengi wazuri kwa sababu ya kushindwa kuishi nao. Ama kwa sababu za mapungufu ya vijana wenyewe au kwa mapungufu ya klabu zetu. Tunashindwa kuvumilia.

Kwa mfano, kama nikitaka mshambuliaji mzuri dirisha dogo lijalo au kubwa lijalo nitasubiri tu pale Simba. Kuna mchezaji mmoja ataachwa kati ya Adam Salamba, Mohamed Rashid au Marcel Kaheza. Sio kwa sababu ya uwezo wao, hapana, wamerundikwa wengi halafu kuna mastaa wengi, halafu sio wote watapata nafasi au kuvumiliwa katika kipindi wanachoizoea klabu taratibu. Matokeo yake kuna mchezaji mzuri ataachwa.

Msimu uliopita Simba ilikuwa imesajili wachezaji mastaa sana. Walianza vizuri hawa kina Jamal Mwambeleko lakini kadri siku zilivyosonga mbele ndivyo ambavyo walianza kuyeyuka taratibu. Hawakuwahi kufikia ubora waliokuwa nao wakati wakiwa klabu zao za awali. Ni Yusuph Mlipili tu ndiye aliyevumiliwa.

Kwa sasa wameondolewa na kurudi katika klabu ambazo watapewa nafasi na kuvumiliwa. Usishangae baada ya miaka miwili Mwambeleko akarudi Yanga au Azam, tena kwa kugombaniwa sana. Kuna kosa kubwa ambalo tunalifanya. Hatupati ubora wa wachezaji hawa kiasi cha kufikia uwezo tuliouona wakati tunawatamani.

Kama mchezaji alikuwa anacheza Mbao kwa asilimia 80 ya uwezo wake, basi anaweza kwenda Simba au Yanga akacheza kwa asilimia 30 tu ya uwezo wake. Kwangu mimi Dilunga niliyemwona Ruvu Shooting ndiye Dilunga ambaye nimemwona Mtibwa. Yule wa Yanga sijui ni nini kilimtokea, lakini nahisi hawakumvumilia.

Mpaka leo naamini kipa wa Singida United, Manyika Peter atarudi katika timu kubwa. Kama sio Yanga basi Azam. Akiwa na Singida amepata maendeleo zaidi kwa sababu amepewa nafasi zaidi na amekomaa kiakili zaidi tofauti na alivyokuwa Simba.

Nilimtazama jinsi alivyodaka katika michuano ya SportPesa pale Kenya niliona wazi alikuwa amekomaa kiakili tofauti na ilivyokuwa Simba.

Hata ukiwauliza watu wa Yanga ni bora kuwa na nani langoni kati ya Manyika na kipa wao, Youth Rostande wangekwambia ni bora kuwa na Manyika.

Hili la kukomaa kiakili ni jambo jingine ambalo wakati mwingine tunafanya makosa kujaribu kuwaadhibu wachezaji ambao hawajakomaa kiakili na kushindwa kuwaelewesha ambacho wanapaswa kukifanya.

Yote haya yanatokana na ukweli hatuendeshi soka letu kwa misingi ya soka la kulipwa.

Hatuna watu wa saikolojia, hatuna watu wa kujua takwimu za wachezaji au kuwaelesha mambo mbalimbali ambayo yanawazunguka.