Hatma ya kesi ya Aveva, Kaburu Oktoba 2

Muktasari:

  • Julai 17, Mwaka huu, Mahakama hiyo, ilitoa siku saba kwa upande wa mashtaka kubadilisha hati ya mashtaka katika kesi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Oktoba 2, mwaka huu, kutoa uamuzi wa kuifuta kesi inayowakabili vigogo wa kabla ya Simba au kuendelea nayo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba amesema hayo leo, Septemba 18, 2018, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha majibu dhidi ya hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi za kutaka kesi hiyo ifutwe.

Septemba 7, mwaka huu, Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko  aliomba  Mahakama hiyo iwafutie mashtaka, washtakiwa hao kwa sababu wameshindwa kuiendesha kesi hiyo.

Nkoko aliwasilisha hoja hiyo, baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa DPP bado hajalipitia jalada la kesi hiyo, kutokana na kuwa katika harakati za kuanzisha Ofisi mpya mkoani Dodoma.

Leo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidia na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, alidai Mahakamani kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi na wako tayari.

Akijibu hoja hizo, Wakili Swai aliomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu bado wanaifanyia kazi amri waliyopewa na mahakama ya kumtafuta Hanspope na Lauwo.

"Bado tunatekeleza amri tuliyopewa na mahakama, lakini kama hiyo haitoshi, Septemba 14, Mwaka huu, naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanawatafuta Hanspope na Lauwo" alidai Swai na kuongeza

"Kitendo cha Takukuru kutoa taarifa za kuwatafuta Hanspope na Lauwo ni moja ya utekelezaji wa amri iliyotolewa na mahakama" alidai Swai.

Kwa upande wake, wakili Kishenyi alidai kuwa juhudi za makusudi zinaonekana za kuwatafuta washtakiwa hao wawili ili waweze kuunganishwa katika kesi hiyo.

"Kwa busara zako, tunaiomba mahakama itupilie mbali ombi lililowasilishwa na upande wa utetezi la kutaka kesi hii ifutwe," alidai Kishenyi na kuongeza

"Tunaomba mahakama ione kuwa juhudi zinaendelea kufanyika kuhakikisha washtakiwa hawa wanapatikana, hivyo itupe fursa ya kuwatafuta na kuwafikishwa Mahakamani badala ya kuifuta kesi" alidai Kishenyi.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko alidai kuwa ombi lao liko pale pale la kuiomba mahakama ifute kesi hiyo, kwa sababu upande wa mashtaka wameshindwa kuendesha kesi.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2, atakapotoa uamuzi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu.

Wengine ni Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Hata hivyo, Julai 17, Mwaka huu, Mahakama hiyo, ilitoa siku saba kwa upande wa mashtaka kubadilisha hati ya mashtaka katika kesi.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Wanadiawa, kuwa Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.