Hata Griezmann amtaka Pogba kukaza uwanjani

PARIS, UFARANSA
STAA Antoine Griezmann amemwambia swahiba wake Paul Pogba kuna njia moja tu ya kuwaziba midomo watu wanaokosoa uchezaji wake ambayo ni kucheza soka la kiwango cha juu.
Pogba amekuwa akishambuliwa kila kona kwa wiki za karibuni kuwa anacheza soka la kichovu ambalo haliendani na thamani ya pesa iliyolipwa na Manchester United kupata saini yake ilipomnasa kutoka Juventus kwa karibu Pauni 90 milioni.
Lakini, Griezmann amemwambia swahiba wake huyo walipokutana kwenye kambi ya Timu ya Taifa ya Ufaransa kwamba acheze mpira ndipo atakapoweza kuwathibitishia vinginevyo watu wanaomsema. Pogba ameanzishwa mara nne tu katika mechi 11 za mwisho za Man United na kumekuwa na ripoti kuwa ametibuana na Kocha Jose Mourinho.
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps alidai Pogba hawezi kuwa na furaha kutokana na hali inayoendelea Man United, lakini Griezmann amekuwa na maoni tofauti.
"Amekuja kwenye timu akiwa na tabasamu pana usoni mwake, alisema Griezmann, ambaye leo Ijumaa usiku anaweza kuwamo kwenye kikosi cha Ufaransa kitakachochuana na Colombia.
"Ameonekana kuwa na furaha. Si kitu rahisi kutocheza kwenye klabu yako na unaona kiwango kimeshuka. Iliwahi kunitokea, hivyo nafahamu vyema."
Pogba hajafunga wala kupiga pasi ya asisti kwenye kikosi cha Man United kwa mechi tisa sasa, tangu alipofanya hivyo kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stoke City, Januari 15 mwaka huu.