Kessy wa Yanga anafanya mambo kisomi balaa!

Muktasari:

  • Mbali na kucheza Yanga, Kessy alizichezea klabu za Simba na Mtibwa Sugar miaka ya nyuma.

Beki wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy amesema, hana habari na 'inshu' ya mkataba wake, licha ya kuwa umeshamalizika kwani suala hilo amemwachia meneja anayemsimamia.

Amesema, anachoangalia ni namna gani anajiweka fiti na sasa ameingia msituni akijifua kwa mazoezi makali ili atakapoambiwa anakwenda timu gani iwe rahisi kwake.

"Kazi ya meneja ni kuhakikisha ananitafutia timu, kazi yangu mimi ni kucheza tu katika kiwango cha juu na ndiyo maana licha ya kutojua msimu ujao nitakuwa wapi hakunifanyi niache kujiandaa kikamilifu,"alisema Kessy lakini bila kutaja jina la meneja wake.

"Mchezaji makini ni rafiki wa mazoezi hata kama hachezi lazima atafanya kwani  mwili wake unakuwa umezoea, nafanya kwa bidii kama vile nacheza mechi kesho ndicho kinachonifanya niamini katika msimu ujao nitakuwa vizuri zaidi."

Alipouliwa kama meneja wake amefanikiwa kupata timu nje zaidi ya Yanga, Kessy amesema: "Kitu kikubwa ninachokiangalia ni maslahi,  kama watatimiza masharti yangu, nitakuwa tayari."