Haji Mwinyi ataka wasipoteze nafasi Shirikisho

Muktasari:

Yanga imepangwa kundi D pamoja na timu za USM Alger ya Algeria, Rayons Sports ya Rwanda na

Gor Mahia ya Kenya.

Dar es Salaam. Beki wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi amewashika 'sikio' wachezaji wenzake na kuwaambia, wakitaka kufanya vizuri hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, wahakikishe hawapotezi nafasi za mabao wanazozipata nyumbani ili mwisho wa siku washinde mechi zao zote.

"Tumekuwa na tabia ya kupoteza nafasi nyingi za wazi za mabao kila tunapocheza hapa nyumbani, jambo linalotusababisha kila tunapokwenda kumaliza mechi zetu za ugenini tusipofanya vizuri tunabaki tunajuta. Tukitaka kufanikiwa katika hatua hii ya makundi ni lazima tuachane na hayo makosa,"anasema Mwinyi.

Kauli ya Mwinyi ni baada ya kupangwa kwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika leo Jumamosi ambapo Yanga ipo kundi D pamoja na timu za USM Alger ya Algeria, Rayons Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya mechi ambazo kwa mujibu wa kalenda zinatakiwa kuchezwa kati ya Mei 6 na kumalizika Agosti 29 na mbili zitakwenda robo fainali.

Safari ya Yanga katika michuano hiyo hadi wanafuzu makundi, walikuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo waliifunga St Luois ya Shelisheli jumla ya mabao 2-1, wakatolewa na Township ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-0, wakashushwa Shirkisho ambako waliitoa Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1.