Guardiola amsuta Mourinho

MANCHESTER, England. BAADA ya Manchester United kupata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa mahasimu wao wa jiji moja Manchester City, kocha wa kambi ya Old Trafford Jose Mourinho aliibuka na tuhuma nzito kwamba wachezaji wa Pep Guardiola kuwa wanacheza kama Barcelona, kwani wanajiangusha mara kwa mara, wakitaka kutoa ushawishi kwa refa.

Lakini Pep kaibuka na kumwambia Mourinho  apambane na hali yake kwa sababu kiungo wa Man United  Ander Hererra ndiye aliyepata kadi kwa kujiangusha katika eneo la penalti.  

"Si kweli kwamba wachezaji wangu huwa wanaanguka kwa urahisi, sidhani kama huo ni mjadala kwa sasa.”

Na wakati Jose Mourinho akisema kwamba City  walishinda mchezo huo kwa bahati, Guardiola anasifia wachezaji wake kwa mziki mnene walioonyesha kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa ikitazamwa na idadi kubwa ya watu duniani.

Guardiola anaamini kwamba maneno ya kocha huyo ni sawa na yale ya mkosaji, haishi kutapatapa na amejigamba zaidi kuwa sasa watu wameshaelewa yeye ni nani katika Ligi Kuu England.

"Msimu uliopiota nilisuasua kidogo, lakini kwa sasa mambo yamenyooka. Kuhusu suala la kucheza kama Barcelona, linawezekana kwa kuwa hakuna anayekatazwa kuchezesha staili anayotaka. Lakini kuhusu kujiangusha, hakuna kitu kama hicho.”

“Ushindi huu ni heshima kwetu. Tumecheza kwa kiwango cha maana na tumepata mafanikio. Siku mbili zijazo tutakwenda kucheza na Swansea nafahamu itakuwa ni kazi ngumu kwani huu ni wakati wa baridi kali.”