Griezmann: Ufaransa hii haina kuremba mwanagu

Muktasari:

  •  Mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid, ameyasema hayo baada ya baadhi ya mashabiki na wachambuzi wa soka kuubeza ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Uholanzi wa mashindano ya Uefa Nations League.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji mahiri wa Ufaransa, Antoine Griezmann amesema wao wanahitaji ushindi tu katika mechi zao na sio kucheza kwa kuremba ili kuwafurahisha mashabiki.

Mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid, ameyasema hayo baada ya baadhi ya mashabiki na wachambuzi wa soka kuubeza ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Uholanzi wa mashindano ya Uefa Nations League.

Alisema hawatajali watu wanaitathmini au kuizungumzi vipi timu yao bali wao wanachokijali ni namna gani wanapata matokeo katika kila mchezo.

“Sisi hatutakia kucheza kama Hispania au kama Barcelona kwa kugonga pasi nyingi, sisi kwa sasa tunaangalia namna gani ya kupata matokeo tunataka ushindi na sio kuwaburudisha watu,” alisema.

Mshambuliaji huyo alisema wanafahamu tangu Ufaransa imetwaa ubingwa wa Dunia, kumekuwa na maneno mengi ya kuwaponda, lakini hayo hayawashughulishi kwa kuwa penye mafanikio vikwazo na chuki huongezeka.

Katika mchezo wa jana mabao ya Ufaransa yalifungwa na Kylian Mbappe na Olivier Giroud aliyefunga bao lake la 32 katika michezo 83 lililomuwezesha kumpiku staa wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane na sasa anashika nafasi ya nne kati ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa hilo.