Gor Mahia yaitumia salamu Yanga Kombe la Shirikisho

Muktasari:

  • Ushindi huo wa mabao 2-0 dhidi ya JKU katika mechi ya mshindi wa tatu Gor Mahia waliondoka hapo wakiwa si mikono mitupu baada ya kutwaa zawadi ya mshindi wa tatu.

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Kenya Gor Mahia hawajaondoka bure katika mashindano ya Kagame Cup baada ya kuwafunga JKU, huku wakijiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga Jumatano wiki ijayo.

Ushindi huo wa mabao 2-0 dhidi ya JKU katika mechi ya mshindi wa tatu Gor Mahia waliondoka hapo wakiwa si mikono mitupu baada ya kutwaa zawadi ya mshindi wa tatu.

Gor Mahia walicheza mechi ya mshindi wa tatu baada ya kupoteza katika mechi ya nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi Azam ambao waliwafunga mabao 2-0 yaliyofungwa na Ditram Nchimbi na Bruce Kangwa.
Wakati JKU wao walifungwa 1-0, katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Simba bao ambalo lilifungwa na Meddie Kagere ambaye amekuwa mwiba katika mashindano haya baada ya kucheza mechi tatu akiwa na mabao matatu.
Gor Mahia licha ya kumaliza mshindi wa pili walichukua ubingwa pia wa kombe la Sport Pesa wakizifunga timu za hapa nchini kama Singida United na Simba katika mechi ya fainali.
Bao la kuongoza la Gor Mahia lilifungwa dakika ya 52 na Francis Mustafa kabla ya dakika ya 89 Samuel Onyango anaifungia Gor Mahia bao la pili baada ya kupokea pasi safi ndani ya boksi kutoka kwa Jacques Tuyisenge.
"Haikuwa siku nzuri kwetu kwani wachezaji wangu wawili wa kikosi cha kwanza walikuwa majeruhi na tulifanya makosa mengi huenda ikawa sababu ya kupoteza mechi hii lakini kwa timu yangu ilivyo nashukuru Mungu kumaliza katika nafasi ya tatu, " alisema kocha wa JKU Hassan Ramadhani.
Baada ya kuondoka kama washindi wa tatu katika mashindano haya huenda Gor Mahia wakawa kama wamewatumia salamu Yanga ambao watakutana nao katika mechi ya kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ambao wataondoka Jumatatu kuelekea Kenya watacheza na Gor Mahia Jumatano katika mechi yao ya tatu baada ya kufungwa dhidi ya USM Alger mabao 4-0 na kutoka sare dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
"Baada ya mashindano haya kumalizika tunakwenda kujiandaa katika mechi ya Shirikisho ambayo tutacheza na Yanga na makosa ambayo nimeyaona kwenye michuano hii yatakuwa kama faida kwetu kuyarekebisha ili kushinda kwani tunacheza kwenye ardhi ya nyumbani, " alisema Dylan Kerr kocha wa Gor Mahia.