Huko Gor Mahia, si salama

Muktasari:

  • Taarifa zinasema, baada ya kupata ushindi wa 5-0 dhidi ya Posta Rangers mjini Kisumu, wachezaji wa Kogalo, waliamua kuvunja kambi yao, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgomo baridi baada ya uongozi wa klabu hiyo kushindwa kuwalipa posho zao.

Nairobi. Siku moja baada ya kushuhudia straika wake wa kutegemewa, Mnyarwanda Meddie Kagere, akihamia Simba SC ya Tanzania, kambi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) huko Gor Mahia, si salama!

Taarifa zinasema, baada ya kupata ushindi wa 5-0 dhidi ya Posta Rangers mjini Kisumu, wachezaji wa Kogalo, waliamua kuvunja kambi yao, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgomo baridi baada ya uongozi wa klabu hiyo kushindwa kuwalipa posho zao.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mgomo huo hauhusiani na mishahara bali malipo ya posho yanayotokana na pesa walizoshinda baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Sportpesa mashindano yaliyomalizika hivi karibuni na Gor Mahia kutetea ubingwa wao walipoifunga Simba kwenye fainali.

Chanzo hicho, kinasema kuwa wachezaji hao walitakiwa kuweka kambi mjini Kisumu kwa ajili ya mechi mbili ya Posta Rangers na ile ya Sony Sugar, inayotarajiwa kuchezwa Ijumaa ya Juni 29, ugani Kisumu, lakini waliamua kuvunja kambi mpaka pale watakapolipwa.

"Mazee kuna tatizo, wachezaji wamevunja kambi, tatizo hawajalipwa posho kutoka kwenye fedha za Sportpesa Super Cup, unajua walikuwa wanapaswa kukaa Kisumu hadi Ijumaa, kwa ajili ya mechi ya Sony Sugar, ngoja tuone venue kutaenda, ila ni ngori," kilisema chanzo hicho.

Uamuzi wa wachezaji hao, unaiweka Gor Mahia katika hali ngumu hasa ikizingatiwa kuwa wana mechi nyingi mbele yao ukiwemo mchezo wa KPL dhidi ya Sony Sugar, michuano ya Kagame Cup, mechi ya kirafiki dhidi ya Everton, nchini England na mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Rayon na Yanga SC.