Gor Mahia, USM Algiers kupigwa Machakos

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza Gor Mahia imefuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika

Nairobi. Hatimaye wawakilishi wa Kenya katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Gor Mahia watautumia Uwanja wa Kenyatta, ulioko mjini Machakos kwa mechi ya kwanza ya nyumbani dhidi ya USM Algiers ya Algeria.

Awali hofu ilikuwa ni uwanja upi watatumia baada ya viwanja vya Nyayo na Kasarani kufungwa kupisha matengenezo kwa muda mrefu, takribani nusu ya msimu, uwanja wa Machakos umekuwa ukitumika.

Gor Mahia watakuwa wenyeji wa USM Algiers katika mchezo wao wa pili wa makundi, Mei 15 baada ya kukutana na Rayon Sports ugenini.

Hata hivyo, licha ya CAF kuridhia uwanja huo utumike, bado kuna shaka na hii ni kutokana na dimba hili kuonekana kuzidiwa hasa ukizingatia kuwa karibu mechi zote za KPL zinachezwa hapo.

Hivi karibuni, uwanja wa machakos ulilazimika kufungwa kwa muda baada ya kuonekana kuwa katika hali mbaya kwa lengo la kuufanyia ukarabati na kama zoezi hilo litachukua muda mrefu kukamilika itabidi Gor Mahia wajipange upya.

Aidha, licha ya kuwa katika hali nzuri na kukubalika kwa mujibu wa baadhi ya sheria za CAF, suala la ulinzi wa ndani na nje ya uwanja bado ni kizungumkuti.

Wakati huo huo, habari njema ni kwamba, kuna kila dalili kuwa viwanja viwili, Kasarani (Nairobi) na Kinoru (Meru), vitakuwa tayari kutumiwa katika ratiba zinazofuata.

Baadhi ya kanuni za uendeshaji wa mashindano za CAF ni pamoja na utayari wa timu mwenyeji. Katika kipengele hicho, CAF huzingatia ubora wa uwanja wa nyumbani kwa klabu shiriki, ubora wa uwanja mbadala, ubora wa viwanja vya mazoezi, Hoteli au sehemu ya kufikia na  maeneo ya huduma ya afya.

Baada ya mchezo dhidi ya USM Algiers, Gor Mahia watawaalika  Yanga ya Tanzania (Julai 17), kabla ya kuwafuata Jijini Dar es Salaam (Julai 27).  Agosti 17, watakuwa wenyeji wa Rayon Sports na kisha wataelekea Algeria kuwakabili USM Algiers (Agosti 28).