Ghafla tu, mambo yalibuma

SIO utani Tanzania imejaliwa kuwa na vipaji vya aina yake katika soka la Tanzania. Achana na miaka ya 1960-90 ambako utamu ulizidi maradufu kwa kushuhudia wakali wa kuupiga mwingi uwanjani. Katika miaka hii ya 2000 kuna mastaa waliofunika kinoma kwa soka lao la kiwango cha juu.

Vipaji hivyo vilitarajiwa labda vingeweza kufika walipofikia kinja Mbwana Samatta, Abdui Banda, Simon Msuva ama Farid Mussa na Thomas Ulimwengu labda kwa kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa uwezo waliokuwa nao.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya wakali hao walizimika ghafla ya michongo ya kucheza nje ya Tanzania ilibaki historia kama utani na baadhi yao kwa sasa ni kama wamesahaulika, ingawa bado wanaendelea kuliamsha katika ligi mbalimbali nchini.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa hao ambao walitikisa kwa vipaji vikubwa walivyonavyo, lakini kwa bahati mbaya hawakwenda mbali na kujikuta thamani zao mbele ya mashabiki zikipungua kiaina, ingawa wanaendelea kupambana walipo.

Athuman Idd ‘Chuji’

Taifa lilimtegemea kutokana na uwezo wake, licha ya kuzichezea klabu kongwe Simba, Yanga kwa nyakati tofauti, pia aliitumikia Taifa Stars. Kwa uwezo aliokuwa nao asingekuwa hapa alipo leo.

Chuji alikuwa kiungo mwenye uwezo wa aina yake, alijua kukaba na kuchezesha timu, alikuwa anapiga mashuti ya umbali mrefu na mengine yalizaa mabao kwa timu yake.

Ajabu Chuji amekuwa akipambana kucheza timu za madaraja ya chini na alifanikiwa kuzipandisha baadhi ya timu kama Mwadui, iliokuwa chini ya Kocha Jamhuri

Kihwelo ‘Julio’ na Coastal Union ya Tanga.

Mrisho Ngassa

Licha ya sasa kupambana kadri awezavyo na akaweza kurejea Yanga ama Simba, lakini kwa soka la kucheza nje ya nchi,litakuwa limemtupa mkono, kwani aliwahi kuchezea ofa zilizokuja mezani kwake.

Ukitaja jina Ngassa kwa wale walimshuhudia enzi zake jinsi alivyokuwa anajua mbio na kuteleza na mpira uwanjani, walimshangaa kukataa ofa kutoka klabu ya El Merreikh, akitaka kuichezea Yanga, iliyo na nyomi ya mashabiki ambao walikuwa wanamuita ‘Anko’.

Mwisho wa picha mambo yakawa magumu kwake,mwaka 2015 akaamua kujiunga na klabu ya Free State ya Afrika Kusini, kabla ya kutimkia Fanja ya Oman ambako pia hakudumu na akajiunga na Mbeya City.

Kwa sasa yupo na Ndanda FC, ambako anapambana kadri awezavyo, kibongo bongo bado anaonyesha ushindani, lakini kuhusu soka la nje ni changamoto kwake.

Haruna Moshi ‘Boban’

Uwezo wake uliwavutia mashabiki na baadhi ya wachezaji kama Shiza Kichuya, Atupele Green, walitamani wafikie kiwango chake ni mchezaji asiye na papara anapokuwa na soka mguuni na anajiamini.

Kwa namna ambavyo Boban alionyesha kiwango cha aina yake, hakustahili kuishia kucheza madaraja ya chini kama ilivyo kwa sasa anavyoitumikia Friends Rangers, ingawa anacheza ligi kuu na kuacha.

Wadau wa soka walijua kipaji cha Boban hasa alipokuwa na Simba na baada ya kuachana na klabu hiyo, alijiunga na Coastal Union kisha akaenda Mbeya City.

Laiti kama Boban angeamua kucheza soka la nje,angekuwa katika mafanikio ya hali ya juu kama ilivyo kwa Mbwana Samatta anayecheza soka Ubeligiji.

Ramadhan Chombo ‘Redondo’

Ni kati ya wachezaji waliowahi kung’ara katika ligi ya VPL, akiwa na Azam na Simba, lakini ghafla kipaji chake kikaanza kufifia taratibu na kuonekana ni mchezaji wa kawaida.

Bado ana uwezo wa kucheza na kupambana, lakini kucheza soka la ushindani nje ya nchi, muda utakuwa umemtupa mkono, tofauti kipindi kile ambapo angefanya maamuzi ya mapema angefika mbali zaidi.

Juma Nyosso

Licha ya kufungiwa hapa na pale na TFF, kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu, bado anaonyesha uwezo wa aina yake uwanjani, lakini si katika kiwango kile alipokuwa na Simba.

Kwa wakati ule Nyosso angeamua kwenda kucheza nje ya nchi, thamani yake ingeendelea kuwa juu, tofauti na sasa licha ya kuitumikia Kagera Sugar,iliyo chini ya kocha Mecky Maxime, ambapo anachukuliwa si ghali.

Said Bahanunzi

Kipaji chake kiliibuka kwa muda mfupi, ghafla kikazima na kubakia kuwa wa kawaida, ndiye alikuwa mfungaji bora mwaka 2012, Yanga Afrika ilipotwaa Kombe la Kagame.

Michuano hiyo ilikuwa kama ya kuaga uwezo wake, tangu hapo Bahanuzi hakuwa kwenye kiwango kizuri, kilichobaki ni stori kwamba aliwahi kucheza Yanga kwa uwezo wa juu.

Jerry Tegete

Alikuwa ni mchezaji bandika bandua kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga na Taifa Stars, iliyokuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo.

Tegete, mtoto wa kocha wa zamani wa Toto Afrika, John Tegete, nyota yake iling’aa kutokana na kazi nzuri aliokuwa anaionyesha uwanjani, ila kwa sasa amebakia kuwa mchezaji wa kawaida.

Kwa sasa anaitumikia Majimaji ya Songea ambako nako hapati nafasi katika kikosi cha kwanza, mara nyingi anaishia kupasha na kukaa benchi.

Kama sio kurejeshwa nchini ili kuwahi pambano la Simba na Yanga, pengine angekuwa anacheza soka la kulipwa Ulaya, ila mambo yalikwama mapema.

Wachezaji hawa baada wapo Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.