Geita Gold yarudi kwa kishindo FDL

Muktasari:

  • Geita Gold SC ambayo itashiriki ligi hiyo msimu ujao baada ya kuinunua timu ya Mshikamano FC uongozi wa Geita Gold umeanika mipango iliyoweka ili kumaliza kiu ya mashabiki na wakazi wa mkoa wa Geita kuwa na timu kwenye Ligi Kuu.

TIMU tajiri na iliyotikisa kwenye Ligi Daraja la Kwanza miaka miwili iliyopita, Geita Gold SC imerejea rasmi kwenye ligi juzi huku ikitangaza mikakati kabambe ya kuhakikisha inacheza Ligi Kuu msimu wa 2019/2020.
Geita Gold SC ambayo itashiriki ligi hiyo msimu ujao baada ya kuinunua timu ya Mshikamano FC uongozi wa Geita Gold umeanika mipango iliyoweka ili kumaliza kiu ya mashabiki na wakazi wa mkoa wa Geita kuwa na timu kwenye Ligi Kuu.
Mratibu mkuu wa timu hiyo, Seif Kulunge, aliliambia Mwanaspoti kuwa baada ya kufanikiwa kuinunua nafasi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza, kinachofuata sasa ni kusuka kikosi chao sambamba na benchi la ufundi.
"Tunamshukuru Mungu hili la kwanza limekamilika na ambacho tunakiangalia kwa sasa ni mchakato wa usajili kwa sababu muda umebaki mfupi lakini jambo jema ni kwamba tayari wenzetu wa Mshikamano walishaanza mchakato wa usajili hiyo tutaendelea pale walipoishia.
Tunaamini nafasi ya kupata wachezaji wazuri bado tunayo na ikiwa tumeshindwa kukamilisha ndani ya muda uliopangwa tutajaribu kuomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) angalau watuongezee muda. Kuhusu kocha mkuu awali tulishazungumza na Juma Mwambusi lakini kwa bahati nzuri akawa amechukuliwa na Azam FC.
Hata hivyo bado wapo makocha wengi wazuri ambao wanaweza kutimiza vyema jukumu la kuhakikisha timu yetu inapanda Ligi Kuu," alisema Kulunge.
Kulunge aliongeza kuwa timu yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha inakuwa na bajeti ya kutosha ya fedha ili iweze kumudu ligi hiyo.
"Geita ni mkoa wa watu waliohamasika. Kama uongozi tumejipanga kukutana na uongozi wa mkoa, wabunge, wafanyabiashara na wananchi wa hapa ili kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuwa na ushiriki mzuri kwenye ligi. Mkoa unapokuwa na timu kwenye Ligi Kuu, unapata fursa nyingi hasa za kibiashara na haitonufaika timu pekee," aliongeza Kulunge.