Cheka aahidi kumpa raha mpinzani wake Shabani Kaoneka

Thursday December 7 2017

 

By Haika Kimaro

Mtwara. Bingwa wa ndondi za kulipwa barani Afrika Francis Cheka anatarajia kupanda ulingoni Desemba 16 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona kuzichapa na Shabani Kaoneka.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Desemba 6 na Cheka wakati akizingumza na waandishi wa habari mjini Mtwara.
Kaoneka anagombea mkanda wa OBO Afrika ambao Cheka anaushikilia kwa miaka mitatu tangu auchukue.
Cheka mwenye asili ya kimakonde amesema ujio wa mpambano huo katika mkoa wa Mtwara ni kukuza na kuendeleza mchezo wa ngumi kwa mkoa wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla na kuutangaza mkoa kitaifa na kimataifa.
Pia, mchezo huo utakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo yatashirikisha mabondia wa mkoa wa Mtwara na mikoa jirani ya ukanda wa kusini ili kujitangaza na kuwahamasisha kucheza mchezo huu kama fursa ya  kujipatia pesa kwani ni kazi kama kazi zingine na kuwafanya vijana kujiajiri kupitia mchezo wa ngumi.
Francis Cheka amejinadi kuwa atampiga mpinzani wake Shabani Kaoneka kwenye mzunguko wa awali kabisa kwa (KO) ili kuendelea kushikiria mkanda huo.
Cheka hajapigana kwa muda mrefu na mchezo huu kwake utakuwa fursa ya kurudisha hadhi yake, na ameomba wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi na mikoa jirani kujitokeza kushuhudia makali yake kwenye ulingo wa Nangwanda Sijaona.