Fifa yaamuru mechi Afrika Kusini, Senegal kurudiwa

Thursday September 7 2017

 

Geneva, Uswisi. Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeamuru kurudiwa kwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2018, kati ya Afrika Kusini na Senegal, iliyopigwa Novemba mwaka jana na Afrika Kusini kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Uamuzi huo unafuatia adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa mwamuzi wa mchezo huo Joseph Lamptey raia wa Ghana anayedaiwa kutia dosari matokeo hayo.

Miongoni mwa dosari ambazo zimebainika kusababishwa na mwamuzi huyo, ni pamoja na kuizawadia penalti Afrika Kusini katika mchezo huo akiashiria kuwa beki wa Senegal ,  Kalidou Koulibaly alikuwa ameunawa mpira.

Kwa mujibu wa FIFA, tukio hilo lilipotazamwa upya kwa kutumia mkanda wa video, ilionekana beki huyo hakuushika mpira bali, mpira ulimgonga kwenye goti na kushangazwa na uamuzi ya mwamuzi ambaye alikuwa karibu na eneo la tukio.

Mchezo huo umepangwa kurudiwa  Novemba mwaka huu wakati  mechi za kimataifa zilizo kwenye kalenda ya Fifa zitakapochezwa tena.