Fei Toto afichua siri Yanga

Muktasari:

  • Feisal na Mo Banka walitua Jangwani kwenye dirisha la usajili la msimu huu, sambamba na kina Deus Kaseke, Heritier Makambo, Mrisho Ngassa, kipa Nkinzi Kindoki na Jaffar Mohammed.

WAKATI mashabiki wa Yanga wakiwa hawajui kinachoendelea juu ya kiungo wao mpya, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ anayedaiwa kusimamishwa kwa tuhuma za kutumia dawa, kiungo mwingine fundi wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefichua siri.

Feisal na Mo Banka walitua Jangwani kwenye dirisha la usajili la msimu huu, sambamba na kina Deus Kaseke, Heritier Makambo, Mrisho Ngassa, kipa Nkinzi Kindoki na Jaffar Mohammed.

Nyota hao wamekuwa na msaada mkubwa Jangwani tangu watue wakiifanya Yanga itofautiane na ile ya msimu uliopita ambayo ilikuwa ikiteseka katika kupata matokeo uwanjani.

Fei Toto amefichua mafanikio ya Yanga ndani ya muda mfupi na kuwapa burudani mashabiki wao imetokana na michongo ya kijanja wanayopewa na Meneja wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Kiungo huyo alisema kwa mfano yeye tangu atue Yanga, amekuwa chini ya ulinzi wa Cannavaro, jambo analoamini limechangia kwa kiasi kikubwa kwenye kiwango cha juu japo bado hawajaanza kuchanganya kwenye Ligi Kuu Bara.

Yanga imecheza mechi moja tu ya Ligi Kuu Bara na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, huku ikicheza mechi tatu za kimataifa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, USM Alger na Rayon Sports ya Rwanda na kushinda moja, kupoteza mbili.

Licha ya kupoteza, lakini soka la Yanga likiwa tofauti na mechi zao za nyuma ikiwamo ile waliopigwa 4-0 mjini Nairobi na Gor Mahia.

Fei Toto aliamua kufichua siri hiyo kutokana na kunaswa mara kadhaa akiwa beneti na Cannavaro wakati mwingine hata kumsubiri meneja huyo anapokuwa kwenye vikao vya utendaji na kulifanya Mwanaspoti kuamua kumuuliza naye akafunguka.

Fei Toto alisema tangu atue Yanga kutoka JKU, amekuwa akikaa pamoja na Cannavaro kwa lengo la kuhakikisha kwamba anafikia mafanikio aliyoyapata nyota huyo ndani ya Yanga.

Alisema sio kwake tu, lakini hata wachezaji wengine ndani ya Yanga wamekuwa wakimuangalia Cannavaro kama kioo chao ndio maana wamekuwa wakijituma na kufanya mambo uwanjani.

“Huyu kwangu na hata kwa wachezaji wengine ni kama kaka, hivyo ninapokaa naye ananifundisha vitu vingi vya mpira lakini pia ananielekeza maisha ya Dar jinsi yalivyo,” alisema Fei Toto.

“Kikubwa tumekuwa tukiota mafanikio kama yake na hata tumpite, ndio maana unaona Yanga imekuwa na moto mkali. Nani hajui Cannavaro amefanya ndani ya Yanga na soka la kimataifa.” Feisal aliongeza, licha ya kukaa na Cannavaro, lakini amekuwa pia akijifunza namna ya kuishi na watu kwani ameona jinsi kaka yake alivyo na ukaribu na kila mtu anayemzunguka.