Fedha zimemaliza mzozo wa Yanga na Azam FC

Muktasari:

Uhasama wa Yanga na Azam ulianza kama mzaha na mwishowe ulichukua sura mpya kwa Yanga kufikia hatua ya hadi kukataa Sh300 milioni za udhamini wa Azam, huku wakidai kutokuwa na njaa.

Dar es Salaam. Miaka kadhaa nyuma kulikuwa na uhasama baina ya Yanga na Azam, ukiachilia mbali ule ambao umezoeleka kati ya Simba na Yanga, ambao upo hadi nje ya uwanja.

Uhasama wa Yanga na Azam ulianza kama mzaha na mwishowe ulichukua sura mpya kwa Yanga kufikia hatua ya hadi kukataa Sh300 milioni za udhamini wa Azam, huku wakidai kutokuwa na njaa.

“Yanga haina njaa, ingekuwa na njaa tungezichukua lakini hatuna njaa na isitoshe hizo fedha hazituhusu, hizo ni fedha za Azam, hivyo wazipangie matumizi mengine,” aliyasema hayo, Jonas Tiboroha, aliyekuwa katibu wa Yanga wakati huo.

Inadaiwa Yanga chini ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Yusuph Manji ilikuwa ikiibeza Azam kuwa ni timu ndogo, ambayo haiwezi kuwababaisha kutokana na ukongwe walionao pamoja na mafanikio waliyojikusanyia.

Huku Azam ikiwa chini ya Yusuph Bakhresa yenyewe ikiivimbia timu hiyo kongwe kwa kuona si lolote mbele yao pamoja na mafanikio makubwa waliyonayo kwenye soka la Tanzania.

Vita ya Yanga na Azam iliendelea nje ya uwanja kwa Yanga kuamua kuachana na matumizi ya maji ya Uhai, ambayo yapo chini ya kampuni ya Azam, hivyo waliingia mkataba na kampuni nyingine ya maji ya Afya.

Baada ya Yanga kuanza kuyumba kiuchumi na hata zama za Tiboroha kupita na ukatibu kuchukuliwa na Charles Mkwasa bila ya Yusuph Manji, ambaye aling’atuka kwenye nafasi yake, ulitoka uamuzi wa kuchukua fedha walizozigomea awali.

“Hatuwezi kuendelea kukataa fedha wakati timu ipo kwenye hali mbaya kifedha,” alisema Mkwasa mara baada ya kukubaliana na Azam.

Hapo ndipo ulikuwa mwisho wa uhasama baina ya Yanga na Azam, wengine wamekuwa wakidai pengine kuondoka kwa Manji kumeifanya Yanga kutokuwa na jeuri tena ya kifedha mbele ya Azam.

Yanga haina tatizo tena na Azam na Jumamosi hii itautumia Uwanja wa Azam Complex kama uwanja wake wa nyumbani watakapocheza na Tanzania Prisons kutokana na Uwanja wa Uhuru kuwa kwenye matumizi mengine.

“Na hata suala la maji pia linadaiwa kufikia kikomo, Yanga imeendelea na matumizi ya maji ya Uhai kama ilivyokuwa awali, Azam nao wanaonekana kutokuwa na neno tena na Yanga.”

Pamoja na yote, imedaiwa katu hakuna uwezekano wa kumaliza uhasama wa Simba na Yanga, ni bora mmoja wao kushuka daraja na kuanza moja kutokana na ukata kuliko kuchukua fungu la fedha kutoka upande mwingine.