Fantastic Four

Monday May 14 2018

 

LONDON, ENGLAND

HABARI ndiyo hiyo. Ile Top Four ya Ligi Kuu England imeshakamilika, lakini habari mbaya Chelsea pointi zake hazikutosha kuingia kwenye kundi hilo la kibabe.

Pazia la Ligi Kuu England lilifungwa rasmi jana Jumapili, huku Mohamed Salah akishinda vita yake na Harry Kane katika kufukuzia Kiatu cha Dhahabu na sasa staa huyo wa Anfield, rasmi ndiye kinara wa ufungaji kwenye ligi hiyo kwa msimu huu baada ya kuwa na mabao 32. Kwenye ile Top Four, zipo Manchester City, ambao ni mabingwa, Manchester United, Tottenham Hotspur na Liverpool, wakati Chelsea na wapinzani wao wa London, Arsenal hawamo kwenye orodha hiyo na sasa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao haitawahusu, watakwenda kucheza kwenye Europa League.

Katika vita ya kushuka daraja, habari ndiyo hiyo imekwisha na sasa Stoke City, Swansea City na West Brom hazitakuwapo kwenye Ligi Kuu England msimu ujao na badala yake zitakwenda kuchuana kwenye Championship.

Chelsea imeliza ligi katika nafasi ya tano, ikivuna pointi 70 katika mechi 38, huku mechi yake ya mwisho ikimalizika kwa aibu ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Newcastle United.

Katika mechi hizo za kufunga pazia la Ligi Kuu hakuna mechi hata mechi moja isiyoshuhudia bao, ambapo Mabingwa, Man City waliichapa Southampton 1-0, bao la dakika za majeruhi la Mbrazili, Gabriel Jesus.

Crystal Palace iliichapa West Brom 2-0, Wilfried Zaha akisukumia mpira wavuni kwenye kipindi cha pili pamoja na Patrick van Aanholt.

Matokeo mengine ya mechi hizo za mwisho wa msimu, ambazo zilishuhudia mabao kibao yakifungwa, Spurs ilitoka nyuma na kuichapa Leicester City 5-4, Kane akipiga bao mbili, wakati Stoke City iliichapa Swansea City 2-1 na Arsenal ikiimpa zawadi ya ushindi kocha wake, Arsene Wenger kwenye mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu England akiwa na timu hiyo baada ya kuichapa Huddersfield 1-0, shukrani kwa bao la Pierre-Emerick Aubameyang.

Liverpool ikiwa Anfield, iliichapa Brighton 4-0, huku Mohamed Salah akiwa mmoja ya waliotupia. West Ham United iliichapa Everton 3-1, Manuel Lanzini akipiga mbili, wakati Man United iliichapa Watford 1-0 huko Old Trafford, bao la kipindi cha kwanza la Marcus Rashford. Burnley ilimaliza ligi kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bournemouth.