FKF, Chapa Dimba kupeleka wachezaji La Liga

Muktasari:

  • Rais wa FKF, Nick Mwendwa amesema, mpango huo unalenga kukuza soka la Kenya ambapo wataalamu kutoka La Liga watashirikiana na makocha nchini kutambua vipaji vya soka na kuwapa mafunzo maalumu kabla ya kwenda Hispania.

Nairobi. Shirikisho La Soka Kenya (FKF), lina mpango wa kuanza mkakati wa kuwauza wachezaji wa ligi mbalimbali kote duniani na  wameingia makubaliano ya kupeleka nyota chipukizi Ligi Kuu ya Hispania, maarufu La Liga.
Rais wa FKF, Nick Mwendwa amesema, mpango huo unalenga kukuza soka la Kenya ambapo wataalamu kutoka La Liga watashirikiana na makocha nchini kutambua vipaji vya soka na kuwapa mafunzo maalumu kabla ya kwenda Hispania.
Akizungumza katika uzinduzi wa msimu wa pili wa mashindano ya kuvumbua vipaji ya Chapa Dimba, maarufu kama ‘Victor Wanyama Cup’, kutokana na kiungo huyo wa Tottenham kuwa Balozi wa mashindano hayo yanayoendeshwa kwa ushirikiano wa FKF, Mwendwa amesema makubaliano yamefikiwa.
Mwendwa alisema, wataalamu kutoka La Liga watazunguka nchi nzima wakati wa mashindano ya Chapa Dimba yanayohusisha vijana wapatao 1500, kuhakikisha wanapata vipaji wanavyovitafuta kutoka katika kaunti zote 47, kote nchini. “Tunafarijika kuona wenzetu kutoka La Liga wamekubali kushirikiana nasi katika harakati za kukuza soka letu.
Katika msimu huu wa pili wa Safari com Chapa Dimba, tutahakikisha tunapata vipaji vingi vya soka.
Tumelenga kukuza soka letu, tunataka kusonga mbele, na hilo litafanikiwa tukiwa na programu kama hizi,” alisema Mwendwa.
Baada ya kupatikana vijana hao watasafiri hadi Hispania kwa ajili ya kambi maalumu ya siku 10, kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na baadhi ya vituo vya kunoa vipaji vya nchini Hispania, ikiwemo kituo cha La Masia, kinachomilikiwa na klabu ya Barcelona, hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa huduma za wateja wa Safari com, Charles Kare.
Kare amesema, mashindano hayo kama ilivyokuwa katika msimu wa kwanza, yatahusisha vijana wenye umri kati ya miaka 16 na 20, ukiwa ni mpango mkakati wa kukuza soka la mashinani.