Everton kumfuata Samatta

Muktasari:

Samatta na Genk yake watafuatwa na Everton, Julai 22 mjini Genk, ikiwa ni siku tisa tu baada ya timu hiyo kucheza na Gor Mahia jijini Dar es Salaam,  yaani Julai 13.

KAMA mshambuliaji, Mbwana Samatta, ataweza kuchanga karata zake vyema dhidi ya  timu ya Everton mwezi ujao, inaweza kuwa ufunguo wa ndoto zake za kucheza Ligi Kuu England iwapo atafanikiwa kuishawishi ipasavyo.

Everton ambayo mwezi ujao itakuwa nchini kucheza na Gor Mahia ya Kenya katika mechi maalumu iliyoandaliwa na kampuni ya SportPesa, imepanga kucheza mechi ya kirafiki na KRC Genk ya Ubelgiji ambayo Samatta anaichezea, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu England.

Samatta na Genk yake watafuatwa na Everton, Julai 22 mjini Genk, ikiwa ni siku tisa tu baada ya timu hiyo kucheza na Gor Mahia jijini Dar es Salaam,  yaani Julai 13.

Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Samatta kucheza dhidi ya timu inayoshiriki Ligi ya England licha ya kukaribia kutimiza ndoto hiyo mwezi Aprili ambapo Genk ilinusa kukumbana na Manchester United katika mashindano ya Ulaya, lakini hilo halikutimia baada ya timu yake kuondolewa na Celta Vigo kwenye hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa kalenda ya mashindano hayo, Everton itaanza rasmi kambi ya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao mwanzoni mwa mwezi Julai kabla ya kuja nchini kukwaana na Gor ambapo baada ya mchezo huo, itaenda Uholanzi itakapocheza mechi ya kirafiki na FC Twente, Julai 19 kabla ya kumalizia na Genk, Julai 22.

Timu hiyo ya Everton inatarajiwa kucheza mchezo wake wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Sevilla, Agosti 6 kabla ya kuingia kwenye mikiki ya Ligi Kuu England ambapo watafungua dimba dhidi ya Stoke City, Agosti 12.