Eti Mwakinyo alikwenda Uingereza kama mwizi

Muktasari:

Mizengwe aliyopata alitaka kumkatisha tamaa ndipo akaamua kutumia njia alizoziita njia za panya hadi kufanikisha safari yake lakini alipotua Uingereza aliamua kuuvaa Utanzania

DODOMA. Bondia Hassan Mwakinyo jana Ijumaa alitua bungeni na mkanda wake kisha akatoa siri nzito ya safari yake nchini Uingereza kwamba alikwenda ughaibuni huko kama mwizi.
Mwakinyo alialikwa bungeni baada ya kushinda mkanda huo katika pambano la utangulizi kwa kumchapa bondia wa Uingereza Sam Eggington kwa TKO ikiwa ni raundi ya pili.
Pambano hilo ambalo lilikuwa la raundi 10 kwa uzani wa Super Welter lilifanyika Mji wa Birmingham, Uingereza ikiwa ni utangulizi wa pambano la ubingwa dhidi ya Amir Khan na Sam Vargas.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Ali Sareh, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harison Mwakyembe aliliambia Bunge kuwa serikali inafahamu kuhusu safari ya bondia huyo na ilikuwa ikifuatilia kwa karibu pambano hilo.
“Kwanza naomba radhi kwa Watanzania na wanamichezo wote kutokana na kauli yangu baada ya mkalimani wangu kule UK, lakini nakanusha vikali kuwa mimi Mwakinyo sikupata ushirikiano wowote kutoka kwa mtu yeyote hata katika safari yangu, ikumbukwe kuwa niliondoka kama mwizi na hata nauli ya kwenda nilikopa hela ya mwanafunzi,” alisema Mwakinyo.
Alisema kibali cha kuondoka kwake nchini kilipatikana kwa shida, kwani hakuna mtu aliyesimama upande wake kumsaidia zaidi ya rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Mbarouk Athuman.

Alisema kuwa mizengwe aliyopata alitaka kumkatisha tamaa ndipo akaamua kutumia njia alizoziita njia za panya hadi kufanikisha safari yake lakini alipotua Uingereza aliamua kuuvaa Utanzania na alijua anapigana kwa ajili ya taifa lake na siyo yeye kama yeye.
Alisema anatamani kukutana na Rais John Magufuli ili amweleze namna ambavyo akina Mwakinyo wengi wanakosa fursa kutokana na urasimu uliopo na masharti na namna ya kusafiri.

APATA MIKATABA MITATU NJE
Mara baada ya kumaliza pambano lake, amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na kampuni za nje ya nchi na tayari hadi jana Ijumaa alikuwa na mikataba ya kampuni tatu za Uingereza.

Hata hivyo alisema hawezi kusaini mikataba hiyo kwani anaamini Tanzania haijashindwa kumpatia mikataba na kumsaidia kujitangaza ili wakati wowote abebe jina la Tanzania.

KUVUNA MKWANJA MWINGINE
Jana Spika wa bunge Job Ndugai alimtangaza Mwakinyo na kuomba kukutana na Waziri Mkuu ili ampe mkono na jambo hilo lilitekelezwa nje ya ukumbi wa bunge ambapo Waziri Mkuu alizungumza naye kisha akamuagiza mbunge wa Tanga mjini ampeleke nyumbani kwake.

Baada ya tangazo la Spika, mbunge wa Sumbawanga Hilaly Aesh aliomba mwongozo akitaka bunge limchangie kila mbunge Sh 20,000 kiwango ambacho kilikubaliwa na wabunge wote.

Licha ukumbi wa Bunge kuwa na wabunge wachache, lakini Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai alisema wabunge watakaochangia ni 393 hata kama hawakuwepo muda huo.

“Bila shaka umesikia kuwa bunge limeazimia, hii ina maana kuwa wabunge wote watachangia, maana imetolewa ndani ya bunge na wote wameafiki kwa hiyo kiasi kitakatwa kwa wabunge 393,” alisema Kagaigai kwa hesabu hizo Mwakinyo jana aliondoka na jumla ya Sh 7,860,000.

AMWAGIWA SIFA KILA KONA
Rafiki wa bodnia huyo ambaye alianza kumsifia hata alipokuwa Uingereza, Mbarouk Athuman, alisema bondia huyo ana kipaji na ni mtu wa kujituma zaidi lakini hapati msaada kutoka kwa mtu yeyote.

Athuman alisema eneo analofanyia mazoezi bondia huyo ni eneo duni katika mazingira ambayo hayakubariki kabisa hivyo akasema akitokea mtu wa kumwendeleza, anaweza kufika mbali.

FOLENI YA 'SELFIE' BUNGENI
Katika lango la bunge, kulikuwa na msururu mrefu wa wabunge ambao walikuwa wakipiga naye picha na kumzonga zaidi kila mmoja akitaka kuzungumza naye.

Mbali na wabunge, waandishi wa habari na watumishi pia waliweka foleni ya kuzungumza na Mwakinyo hata iliwalazimu baadhi ya watu kumtoa kwa nguvu na kumpeleka katika mgahawa wa bunge ingawa bado alikutana na hali hiyo hiyo baada ya Naibu Waziri wa ardhi Anjelina Mabula kupiga naye picha, likazuka kundi kubwa la wabunge na watumishi wa mgahawa nao wakitaka picha ya pamoja.

KUTUA TANGA
Mwakinyo anatarajiwa kutua jijini Tanga leo Jumamosi ambako ndiko nyumbani kwao na imeelezwa kwamba ameandaliwa mapokezi makubwa kutoka na ushujaa aliouonyesha Uingereza.