Eti! Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kupigwa Marekani

Muktasari:

  • Imefichuliwa kuwa upo mpango na mazungumzo yamefikia hatua ya juu, kuhakikisha mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya unachezwa Marekani kama  ilivyokuwa kwa baadhi ya michezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

Paris, Ufaransa. Wakati tayari fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019 zikiwa zimepangwa kupigwa katika mji wa Madrid nchini Hispania, hizo zinaweza kuwa fainali za mwisho katika miaka ya hivi karibuni, kuchezwa ndani ya Ulaya.

Imefichuliwa kuwa upo mpango na mazungumzo yamefikia hatua ya juu, kuhakikisha mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya unachezwa Marekani kama  ilivyokuwa kwa baadhi ya michezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

Lengo la kuhamisha mechi hizo za fainli ni kuwahamisha wamarekani kupenda soka kwa upande mmoja na upande wa pili Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) likihitaji kujinufaisha kiuchumi kutokana na mapato ya viingilio na matangazo ya kibiashara.

Gazeti la London Evening Standard la Uingereza pamoja na kituo cha televisheni mjini Barcelona na Ràdio's 'El Mati ya Catalunya, nchini Hispania vimefichua juu ya mpango huo huku mtendaji mkuu wa Tv ya Mediapro iliyopo Barcelona, Jaume Roures, akisema anao ushahidi wa kutosha.

Roures alisema kuwa maafikiano ni kuwa mechi ya fainali ya mwaka 2020 au 2021 zipigwe mjini New York na zinazofuata zipigwe kwenye miji mingine ya Marekani.

“Kwa namna mazungumzo yalipofikia ni wazi kwamba fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2020 zitachezwa nje ya bara la Ulaya, itachezwa mjini New York,” alisema.

Roures alisema kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona ipi itawahi ni fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya au michezo kadhaa ya Ligi Kuu Hispania.