Enyimba, USM Alger kikwazi kwa Yanga

Muktasari:

  • Yanga haijawahi kufuzu kwa robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika

Dar es Salaam. Yanga inasubiri ratiba ya hatua ya makundi itakayopangwa katika makao makuu ya CAF, Cairo, Misri, kesho Jumamosi, 21 Aprili 2018, Saa 9:00 Alasiri moja ya wapinzani wake watakuwa kati USM Alger (Algeria), Al Hilal (Sudan), AS Vita (DR Congo) na Enyimba (Nigeria).

Mabingwa hao wa zamani wa Afrika, USM Alger, Al Hilal, AS Vita na Enyimba wamepangwa chungu cha kwanza hivyo ni lazimi Yanga itapangwa na mmoja ya timu hizo kati ya tatu watakazokuwa nazo katika kundi mmoja.

Chungu cha pili kitakuwa na timu 12 ambazo ni : CARA (Congo), ASEC Mimosas (Ivory Coast), Williamsville A.C (Ivory Coast), Al Masry (Misri), Aduana Stars (Ghana), Gor Mahia (Kenya), Djoliba (Mali), RS Berkane (Morocco), Raja Club Athletic (Morocco), UD Songo ( Msumbiji), Rayon Sport (Rwanda), Yanga (Tanzania).

Timu hizo 16, zitagawanywa katika makundi manne: A, B, C, D, katika droo hiyo zitaanza kupangwa timu za chungu cha pili.

Timu itakayopangwa ya kwanza itakwenda moja kwa moja katika Kundi A. Droo itafanywa kuamua nafasi yao (A1, A2, A3 au A4)

Timu itakayochaguliwa ya pili itakwenda Kundi B. Droo itafanywa kuamua nafasi yake (B1, B2,

Timu itakayochaguliwa ya tatu itakwenda Kundi C. Droo itafanywa kuamua nafasi yake (C1, C2, C3 au C4)

Timu itakayochaguliwa ya nne itakwenda Kundi D. Droo itafanywa kuamua nafasi yake (D1, D2, D3 au D4)

Utaratibu huo utarudiwa hadi timu zote za Chungu cha pili zitakapomalizika. Ndipo timu za Chungu cha kwanza nazo zitarudia kupangiwa katika makundi hayo kukamilisha idadi ya timu hizo.

Habari njema kwa Yanga timu nane zilizofuzu kwa hatua hiyo zimefuzu kwa mara ya kwanza hivyo ugenini huo unawapa nafasi mabingwa hao wa Tanzania bara kufanya vizuri iwapo watajipanga vizuri.

Timu zinazocheza kwa mara ya kwanza ni Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda, Aduana (Ghana), Williamsville (Ivory Coast), UD Songo (Msumbiji), El Masry (Misri) na RS Berkane (Morocco).

Pia, hatua hiyo kutashudia mabingwa wa zamani wa Afrika, AS Vita (DR Congo), Raja Club Athletic (Morocco), ASEC Mimosas (Ivory Coast) na Enyimba (Nigeria). CARA (Congo) pia iliwahi kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1974, nayo inafuzu kwa mara ya pili. Miamba mingine ni Djoliba ya Mali, USM Alger (Algeria), na El Hilal (Sudan).

Yanga kwa kufuzu kwa hatua ya makundi imepata dola 275,000 (Sh 616 miloni ) na kuichangia TFF dola 13, 750 (Sh30.8 milioni).

TFF inategemea kupata mgao wa dola 17500 (Sh 39.2 milioni), iwapo Yanga itafuzu kwa robo fainali itapata dola 350,000 (Sh 785milioni). Kama itafuzu kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho itapata dola 450,000 (Sh1bilioni) itaichangia TFF dola 22,500 (Sh 50.4 milioni).

Iwapo Yanga itafanikiwa kucheza fainali itakapotwaa ubingwa itaingiza dola 1.25 milioni (Sh2.8 bilioni), TFF itaondoka na dola 62,500 (Sh 140.1milioni), lakini kama Yanga watamaliza nafasi ya pili,  TFF itaweka mfukoni dola 31, 250 (Sh 70milioni) wakati miamba hiyo ya Jangwani watafunga mwaka na dola 625,000 (Sh.1.4bilioni)