Duh, eti Ali Gulam kajichanganya!

HII kweli kali ya mwaka! Pamoja na jitihada zote za mwanariadha Aliy Gulam hadi kushiriki Michezo ya Madola kule Australia bado kaambiwa eti ni kazi bure.

Gulam anayechuana kwenye mbio fupi za mita 100 na 200 amepewa makavu na aliyekuwa kocha wake alipokuwa kambini nchini Brunei, Suleiman Nyambui.

Kigogo huyo ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Brunei, amemwambia Gulam kuwa kwenye mbio za mita 100 na 200 ambazo anachuana hivi sasa eti hakumfai.

“Nilimwambia hata alipokuwa Brunei kambini, mbio hizo itamchukua muda kufanya vizuri, nilimshauri akimbie mbio za mita 400 na 800, lakini sijui mwenyewe mipango yake,” alisema Nyambui.

Alisema Gulam atafiti kwenye mbio za mita 400 na 800 tofauti na zile za mita 100 na 200 anazokimbia sasa.

“Kwenye mita 100 na 200 kunahitaji mkimbiaji anayenyumbulika mno, Gulam hayuko hivyo, inabidi akubali kubadili mbio ili afanye vizuri kwani umri unamruhusu.”

Mwanariadha huyo Mzanzibar aliishia katika hatua ya mchujo katika michezo hiyo ya Madola iliyofanyika mwezi uliopita. Katika mashindano hayo, Tanzania haikuambulia chochote kwa wanamichezo wake hawakuonyesha maajabu tofauti na mataifa mengine.