Duh! Hebu sikia kisa cha hawa mabondia

KAMA ni dhuluma basi hii imepitiliza aisee. Inawezekanaje hii? Yaani promota anamsafirisha bondia kwenda kuzichapa nje ya nchi, halafu eti anamlipisha hadi hela ya kutumia maliwato ya ndege!

Sasa katika ngumi za Bongo hilo sio ishu kabisa, yaani kuna mapromota si tu wanawatoza mabondia fedha ya kutumia vyoo vya ndege, bali hadi vyakula ndani ya ndege hizo wanapokwenda majuu, wakati hizo huduma hutolewa bure kwa abiria. Yaani hadi aibu bana.

Ishu hiyo ilibainika juzi Jumanne pale ilipoibuliwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

“Ngumi zetu zilipofikia ni aibu, hivi kweli promota unampeleka bondia kupigana nje halafu unamtoza chakula cha kwenye ndege? Na huduma ya choo? Huu ni uonevu mkubwa,” alisema Mwakyembe aliyekutana na wadau wa ngumi ili kupata mrejesho wa mikakati ya maendeleo ya ngumi.

“Mabondia wengine wanapigwa ngumi za vichwani hadi wanapata matatizo, lakini bado mnawadhulumu, nimeshaambiwa hili na taarifa zake zote ninazo. Kuanzia sasa mikataba ya mabondia wanaokwenda kupigana nje sharti iwe wazi.”

Pia, hakuishia hapo amewaonya pia vigogo wa vyama vya ngumi nchini; Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustadhi’ na Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa, kuwa wajitathimini kwa tuhuma zinazowakabili za kuvuruga ngumi za kulipwa nchini.

Awali, katika mkutano huo, wadau wa ngumi waligawanyika; kundi la kwanza liliwahusisha Team Ustadh na Team Mlundwa huku jingine likimsapoti, Emmanuel Salehe, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati iliyopewa mamlaka ya kusimamia ngumi na Dk. Mwakyembe aliwatuhumu wawili hao kupinga mikakati ya serikali ya kuimarisha mchezo huo.