Dua ya mama siri ya ushindi wa Mwakinyo

Muktasari:

Bondia huyo kwa mara ya kwanza ameshinda katika pambano lake alilocheza nje ya Tanzania

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ametua Dar es Salaam na kuweka wazi siri ya ushindi wake ni dua aliyopewa na mama yake kabla ya kuondoka nchini.

Mwakinyo amerejea alfajiri ya leo Ijumaa akitokea England alipomchapa bondia Muingereza Sam Eggington kwa TKO katika raundi ya pili katika pambano la raundi kumi la uzito wa Super Welter.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Mwakinyo alisema mafanikio yake yametokana na Baraka za mama yake.

Mwakinyo alisema wakati anaondoka alipokea baraka kutoka kwa mama na ndipo akaanza safari.

“Mama alinipa kitu kikubwa ambacho ni dua ya ushindi na safari iwe ya kheri kwangu, dua ndio kila kitu kwa sababu Mungu ndio muweza wa yote na nashukuru Mungu nimefanikiwa.”

ANASA HAZIPI NAFASI

Kama kulikuwa na watu wana mmendea bondia huyu baada ya kupata jina kubwa na kumtamani kimwili basi wanajiongopea kwani jamaa siyo mtu wa mambo hayo.

Mwakinyo wakati anashuka katika Ndege alikuwa ameshikilia kitabu cha dini (Msaafu), huku sura yake ikiwa inatabasamu zito kutoka moyoni.

Alifunguka yeye sio mtu wa anasa hata kidogo na hata watu wake wanaomzunguka siyo watu wa namna hiyo hivyo haamini kama anaweza kubadilika.

“Nimelelewa katika mazingira ya dini na hata watu ambao wananizunguka mimi ni watu wa dini, muda wangu mwingi nautumia katika mazoezi kwahiyo siamini kama hivyo vitu nitakuja kuvipa nafasi kwangu.”

SERIKALI YATIA NENO

Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Maendeleo idara ya michezo Yusuph Singo aliyefika uwanjani hapo na kumpokea alisema watahakikisha bondia huyo atatetea mkanda wake akiwa nyumbani.

“Tunampongeza kijana kwamba amefanya vizuri na salamu hizi zimetoka kwa Waziri Mwakyembe, tutahakikisha mkanda huu atatutetea akiwa hapa nyumbani ili aweze kuibuka na ushindi,” alisema Singo.