Donald Ngoma atimkia Azam

Muktasari:

Taarifa za Ngoma kusaini kuichezea Azam FC zilianza kutikisa saa chache kabla ya waumini wa dini ya Kiislamu kupata futari na mmoja wa mabosi wa klabu hiyo ndiye aliyefanikisha usajili huo.

Dar es Salaam: Msimu ujao nakwambia patachimbika ndani ya Ligi Kuu Bara. Mabosi wa Azam FC wanajaribu kukanusha kumsainisha straika matata wa Yanga, Donald Ngoma, lakini taarifa zinafichua kwamba Mzimbabwe huyo tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja kukipiga pale Chamazi Complex.
Taarifa za Ngoma kusaini kuichezea Azam FC zilianza kutikisa saa chache kabla ya waumini wa dini ya Kiislamu kupata futari na mmoja wa mabosi wa klabu hiyo ndiye aliyefanikisha usajili huo.
Hatua hiyo, inakuja kufuatia Ngoma kusitishiwa mkataba na Yanga baada ya klabu hiyo kuishiwa uvumilivu kwa mchezaji huyo, ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha kwa muda mrefu na kushindwa kuonekana uwanjani kwa Zaidi ya nusu na robo za mechi za timu hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' amethitisha jana kuwa klabu yake ilikuwa na mazungumzo na Ngoma, lakini kuhusu kusaini bado mshambuliaji huyo hajasaini.
"Ngoma bado hatujamsainisha na kama itatokea hivyo basi tutatoa taarifa rasmi kwa umma na hakutakuwa na siri hata kidogo," amesema Popat.
"Kilichopo ni kuwa leo tumekutana naye na kufanya mazungumzo, lakini hatujamalizana na pande zote zimeondoka na kile tulichozungumza. Nadhani tusubiri kuona nini kitatokea," alisema.