Dogo wa Madola ana hesabu mpya

Muktasari:

Michezo hiyo itafanyika Goldcoast, Australia.

UNAMKUMBUKA yule dogo, Damas Damian aliyechukua medali ya shaba kwenye mbio za Jumuiya ya Madola ya vijana? Basi bwana mdogo huyo kumbe katulia zake tu pale Mbulu akisubiri wakati ufike.

Mwanariadha huyo yupo kambini akipiga tizi la maana kuisubiri Aprili ya mwakani ifike ili aende tena akachukue medali nyingine kwenye michezo hiyo, lakini sasa akitaka medali ya wakubwa. Michezo hiyo itafanyika Goldcoast, Australia.

“Nasubiri tu vigezo vya TOC (Kamati ya Olimpiki Tanzania) kwani kuanzia mwakani nitakuwa na sifa za kushiriki michezo ya wakubwa, nataka niende nikalete medali nyingine,” alisema Damian.

Mjomba wa Damian ambaye ndiye alimwingiza kwenye riadha, Meta Petro,  alisema dogo huyo kambini hapo ananolewa na Kocha Francis Nade.

“Kambini hapo kuna wanariadha wengine kadhaa na mazoezi yake yanaendelea vizuri, tunamuandaa kwa ajili ya Madola,” alisema.