Djokovic atwaa taji la 14 la Grand Slam

Muktasari:

  • Djokovic mwenye miaka 31 alishinda mchezo wa fainali kwa 6-3 7-6 (7-4) 6-3 na sasa anashika nafasi ya tatu kwa kutwaa mataji mengi akilingana na Pete Sampras, waliomzidi ni Roger Federer mwenye mataji 20 na Rafael Nadal mwenye mataji 17 ya Grand Slam.

New York, Marekani. Mcheza tenisi mahiri wa Serbia, Novak Djokovic ametwaa taji lake la 14 la Grand Slam, baada ya kumshinda Juan Martin del Potro katika fainali ya US Open 2018.

Djokovic mwenye miaka 31 alishinda mchezo wa fainali kwa 6-3 7-6 (7-4) 6-3 na sasa anashika nafasi ya tatu kwa kutwaa mataji mengi akilingana na Pete Sampras, waliomzidi ni Roger Federer mwenye mataji 20 na Rafael Nadal mwenye mataji 17 ya Grand Slam.

Mchezaji huyo anayeshika nafasi ya kwa ubora duniani alitwaa mataji sita ya Australian Open miaka ya 2008, 2011, 2012, 2013, 2015, 2016, French Open mwaka 2016, Wimbledon miaka ya 2011, 2014, 2015 na 2018 na US Open 2011, 2015 na 2018.

Djokovic, aliyetwaa ubingwa wa Wimbledon Julai mwaka huu, ushindi umempandisha nafasi ya tatu kwa ubora akitokea nafasi ya saba katika viwango vya ubora wa tenisi.

Del Potro, raia wa Argentina mwenye miaka 29, alikuwa akicheza mchezo wa kwanza wa fainali ya Grand Slam tangu mwaka 2009 alipotwaa taji la US Open.

Katika mchezo huo uliofanyika Flushing Meadows, Djokovic, alithibitisha kuwa amepania kurejesha ubabe wake uliomuwezesha kuwa namba moja kwa ubora duniani.