Dilunga apiga mbili Mtibwa fainali

Muktasari:

Bingwa wa mashindano hayo anapata tiketi ya kuchezo Kombe la Shirikisho Afrika


Shinyanga. Mtibwa Sugar imekuwa timu ya kwanza kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho FA baada ya kuifunga Stand United mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kiungo Hassan Dilunga alikuwa shujaa wa Mtibwa Sugar baada ya kuifungia timu yake mabao yote mawili dakika ya 30 na 39.

Katika mchezo huo, Mtibwa Sugar walitawala kuanzia mwanzo wa mchezo wakionyesha wamepania kufika fainali ambako bingwa wa mashindano hayo atapata Sh50milioni atakayemaliza nafasi ya pili atajinyakulia Sh10milioni.

Licha ya kipindi cha pili Stand kujaribu kutaka kusawazisha mabao hayo,haikuweza kuambulia chochote kwani hatari zote ziliishia miguuni mwa mabeki wa timu pinzani na nyingine kushindwa kuzifanyia kazi kutokana na hali ya uwanja kujaa tope.

Kutokana na matokeo hayo, Mtibwa Sugar itacheza fainali na mshindi kati ya Singida United na JKT Tanzania mchezo utakaochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Namfua Singida.

Fainali ya Kombe la FA mwaka huu imepangwa kufanyika Juni 2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.