Diego Simeone amkataa mwanae

Muktasari:

  • Mtoto huyo ameonyesha kiwango cha juu katika kikosi cha Argentina hivi karibuni

Madrid, Hispania. Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amesema hana mpango wa kumsajili mwanae wa kumzaa Giovanni Simeone, licha ya kuwa na kiwango bora kwa sasa.

Simeone alimmwagia sifa mwane huyo mwenye miaka 23 ambaye ni mshambuliaji akisema kwa sasa amekamilika kiuchezaji, ingawa yeye hana mpango naye.

“Kwa hakika hivi sasa Giovanni anacheza soka la uhakika nimekuwa nikimfuatilia katika timu yake ya Fiorentina aliyojiunga nayo akitokea Genoa pia ya Italia mwaka jana,” alisema.

Aliongeza kuwa wakati akitua Genoa akitokea River Plate ya Argentina Agosti 2016, alikuwa anahitaji kujifunza mambo mengi ili kuwa mchezaji bora lakini kwa sasa amekamilika na anaweza kucheza kwenye klabu yoyote ile.

Giovanni aliifungia Genoa mabao 13 msimu uliopita na kuishawishi Fiorentina kutoa Euro 18 milioni Agosti 2017 na akalipa fadhila kwa kufunga mabao 15 katika mechi 41 alizoitumikia msimu uliopita.

Alisema anachotamani kwa sasa kukiona kwa mwanae ni kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina lakini sio kumsajili ili aitumikie Atletico kwa kuwa kufanya hivyo kutawapa wote wawili mazingira magumu ya ufanyaji kazi.