Dida, Manula waipasua Simba

Muktasari:

  • Iwapo Simba itaamua kumpa kila kipa nafasi, maana yake Dida na Manula watapata muda mdogo wa kucheza jambo ambalo lina athari kwa muendelezo wa vipaji vyao.

Dar es Salaam. Hapana shaka yoyote kwamba Deogratias Munishi 'Dida' na Aishi Manula ni miongoni mwa makipa bora watano wazawa hapa nchini kwa sasa wakiungana na Juma Kaseja, Aaron Kalambo na Benedictor Tinoco.

Kocha yeyote anayehitaji kufanya vizuri kwenye ligi na mashindano ya ndani au yale ya kimataifa, bila shaka atapenda kuwa na Dida ama Manula kwenye lango lake kutokana na uzoefu na kiwango bora ambacho wawili hao wamekuwa wakionyesha pindi wanapokuwa wanalinda nyavu za timu zao.

Baada ya kuonja mafanikio msimu uliomalizika ikiwa na Aishi Manula iliyemnasa kutoka Azam FC, katika dirisha hili la usajili, Simba imeamua kuimarisha zaidi safu yake ya ulinzi kwa kumsajili Dida jambo linalofanya iwe na makipa wawili bora ndani ya kikosi chake.

 

Usajili wa Dida ambao Simba imeufanya, una faida kubwa kwao kwani utasaidia kuimarisha kiwango cha Manula ambaye sasa atalazimika kufanya kazi ya ziada ili ajihakikishie nafasi kwenye kikosi cha kwanza tofauti na msimu ulioisha ambao hakuwa na mpinzani.

Lakini pia uwepo wa Dida unaipa uhakika Simba wa kutotetereka pindi Manula atakapoumia kwani kipa huyo wa zamani wa Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar ana ubora wa daraja la juu unaoenda sambamba na mwenzake aliyemkuta tofauti na makipa wengine waliopo kwenye kikosi cha Simba, Said Mohammed 'Nduda', Emmanuel Mseja na Ally Salim walioshindwa kabisa kumletea upinzani Manula.

Hata hivyo wakati Simba ikionekana imelamba dume kwa kumchukua Dida, usajili huo unafanya hatima ya kipaji cha kipa huyo pamoja na Manula kuwa kama asali iliyo katika ncha ya kisu ambayo ulimi wa mwanadamu unataka kuilamba.

Hesabu za mlamba asali zikienda vizuri maana yake atafanikiwa kufaidi utamu wa asali hiyo lakini hali ikiwa tofauti maana yake atajikata ulimi.

Manula ni kipa namba moja wa Simba na tayari ameshafanikiwa kujenga imani yake kwenye bechi la ufundi la timu hiyo.

Maana yake kuna uwezekano mkubwa wa Dida kuwa kipa wa akiba wa Simba katika msimu ujao wa ligi na kutokana na utamaduni uliojengeka mara kwa mara wa makocha kutopenda kufanya mabadiliko kwenye nafasi ya kipa, maana yake huenda Dida anaweza kujikuta akisotea benchi na kupelekea kiwango chake kutetereka.

Lakini kama Dida atafanikiwa kuwa chaguo la kwanza, maana yake hiyo itasababisha Manula kusotea benchi na inaweza kusababisha kuporomosha kiwango chake katika umri wake mdogo na kuzima ndoto zake za kufika mbali kisoka.

Iwapo Simba itaamua kumpa kila kipa nafasi, maana yake Dida na Manula watapata muda mdogo wa kucheza jambo ambalo lina athari kwa muendelezo wa vipaji vyao.

Ingekuwa ni wachezaji wanaocheza nafasi za ndani, usajili wa Dida wala usingeleta sintofahamu na hofu kwa sababu ni rahisi kwa mchezaji wa ndani kufanyiwa mabadiliko mara kwa mara.

Lakini kutokana na ugumu wa nafasi ya kipa kufanyiwa mabadiliko. Usajili wa Dida unaweza kuwa mwanzo wa anguko lake au ukawa sababu ya kuporomosha kiwango cha Manula.

Ni suala la kujipa muda na kuona nini kitatokea.