Dayna atoa siri ya kujitoa kwa Shedy Clever

Thursday September 7 2017

 

By FRANK NGOBILE

Dar es Salaam. Mwanamuziki Dayna amefunguka kuhusiana na ishu iliyomfanya kusitisha mkataba wa kufanya kazi na produza Shedy Clever ambavyo kazi zake nyingi zilikua zikitokea huko.

Katika mahojiano na MCL Digital, Dayna alisema kwa sasa hafanyi kazi na produza huyo kutokana na kutofautiana baada ya kumpa biti yake msanii mwingine kuifanyia kazi.

“Shedy alimpa biti langu Diamond Platnumz la wimbo wa My Number One bila kunipa taarifa yoyote ile, mimi nilipewa taarifa na mtu kwamba huku Shedy yupo anafanya hili jambo na Diamond kwa siri ili mimi nisijue.”

“Sasa kwa hali kama hiyo na mtu ambae nilimuamini akafanya kitendo kama hicho mimi nikaamua kuachana naye na nashukuru Mungu nikapata Produza mkali Mr T,”.

Aidha Dayna aliongeza kutokea kwa jambo hilo lilimvunja moyo kwa upande Fulani, lakini sasa yupo vizuri na amekwisha sahau kabisa na ndio maana anaendelea kupiga kazi kama kawaida.

“Pengine Mungu ana makusudi yake pia, mfano sasa nipo kwenye Tuzo za Afrimma na nimezidi kuongeza mashabiki zaidi na zaidi tofauti na kipindi cha nyuma.”

Kuhusu kolabo za nje Dayna anasema mashabiki walikua wakimuomba kufanya kolabo za nje, lakini kwake alikuwa akiona muda bado wa kufanya hivyo sababu hakutaka kufanya kolabo ili mradi kafanya tu.

“Kuna siku Yemi Alade alinipost watu wakaanza kusema hapa hapa Dayna atatumia fursa, lakini kwangu nilikuwa bado na malengo mengine sikuwa tayari kwa kolabo za nje, lakini kwa sasa nimejipanga kuja kumaliza kabisa na hizo kolabo na mikakati imeshaanza muda kwa sasa kuna wimbo nimefanya na produza mmoja mkubwa Afrika Kusini,” aliongeza zaidi

Kupitia video yake mpya ya wimbo wa Chovya ambayo anasema ndiyo ya kwanza kufanyika nje ya Bongo amethibitisha kuhusu video vixen aliyeonekana katika video hiyo ambapo amethibitisha kuwa ni kweli ni mdogo wa Drake kama baadhi ya taarifa zinavyosema.

“Ni kweli yule ni mdogo wa Drake anaitwa Kylie na kwa jinsi tulivyokutana ni kama bahati tu hivi na nakiri wazi sijamlipa chochote ila kuna mambo ambayo walikubaliana na uongozi akakubali kushiriki katika video,”

“Sina mazoea naye kihivyo maana wabongo hatukosi mambo, sababu ni mtu ambae yupo bize sana na mambo yake japo tunawasiliana kidogo kidogo, lakini ndio hivyo mnavyoona kashiriki katika video yangu najua itakuwa kuna maeneo imefika mbali zaidi,” alisema Dayna.