Dar, Tabora, Pwani zavuna dhahabu Umisseta

Muktasari:

  • Wanariadha, Frola Samwel na James Kajana wa Tabora wameibuka vinara katika fainali ya kurusha tufe katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na kampuni ya Coca Cola Tanzania.

Mwanza. Wanariadha wa mikoa ya Tabora, Pwani na Dar es Salaam wametangulia kutwaa medali za dhahabu katika mashindano ya Cops Umisseta yanayoendelea mjini hapa.

Wanariadha, Frola Samwel na James Kajana wa Tabora wameibuka vinara katika fainali ya kurusha tufe katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na kampuni ya Coca Cola Tanzania.

Frola aliibuka kinara katika fainali ya tufe akirusha umbali wa mita 9:58 huku Kajana akitwaa dhahabu upande wa wanaume akirusha umbali wa mita 11:90.

"Tulijiandaa kushinda, huu ni mwanzo tu, tumejipanga kuchukua medali nyingine pia katika mitupo (kisahani na mkuki)," alisema Kajana muda mfupi baada ya kutwaa ubingwa kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba.

Medali nyingine ya dhahabu ilichukuliwa na Regina Mpigachai wa Pwani aliyeshinda kwenye fainali ya mbio za mita 1500.

Regina alitwaa medali hiyo akitumia dakika 4:47:53 huku Epmack Boniface wa Dar akitwaa medali kama hiyo upande wa wavulana akitumia dakika 4:06:51.

Nafasi ya pili  ilichukuliwa na Mbaraka James wa Tanga aliyekimbia kwa dakika 4:09:35 na Deogratius Daud alimaliza wa tatu akikimbia kwa dakika 4:09:94.

Upande wa wasichana, Zayaa Mbadule wa Iringa alimaliza wa pili akikimbia kwa dakika 4:07:35 na Pashuliwa Alex alimaliza wa tatu akikimbia kwa dakika 4:56:47.

Kwenye Tufe, nafasi ya pili ilichukuliwa na Neema Modest wa Manyara aliyerusha umbali wa mita 9:19 na Mariam Henry wa Shinyanga alimaliza wa tatu akirusha umbali wa mita 9:17.

Upande wa wavulana, Ibrahim Haji wa Mwanza alimaliza wa pili akirusha umbali wa mita 11:40 na Deogras Manene alimaliza wa tatu akirusha umbali wa mita 11:02.

Kwenye netiboli timu ya mkoa wa Morogoro iliichakaza Kagera kwa magoli 45-15 katika mchezo wa hatua ya makundi uwanjani hapi.

Katika Soka la wasichana, bingwa mtetezi Dar es Salaam alijiwekea mazingira mazuri ya kutinga robo fainali baada ya kuifunga Geita mabao 4-0.

Mabao ya Dar es Salaam yalifungwa na Joyce Meshack aliyefunga matatu na beki Kija Kassian.

Katika Kikapu Kagera tena ilikubali kipigo cha pointi 43-11 dhidi ya Mara katika mchezo wa makundi.