Dante: Nyie chongeni, ila tutawanyoosha

Muktasari:

  • Yanga inayosubiri kujua itapangwa na nani katika mechi ya mchujo kuingia makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika katika droo itakayofanyika kesho, itacheza mechi yake hiyo kati ya Aprili 6-8, hivyo kutibua pambano la watani.

MASHABIKI wa Simba na Yanga wamekatwa stimu baada ya kubaini kuwa pambano la timu zao halitakuwepo tena Aprili 7, hii ni baada ya Yanga kuendelea na majukumu yake ya mechi za kimataifa.

Yanga inayosubiri kujua itapangwa na nani katika mechi ya mchujo kuingia makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika katika droo itakayofanyika kesho, itacheza mechi yake hiyo kati ya Aprili 6-8, hivyo kutibua pambano la watani.

Hata hivyo, kumbe wakati pambano hilo likiota mbawa kwa mara ya tatu mfululizo kabla ya kuchezwa kwake, beki Andrew Vincent ‘Dante’ amewasikia wapinzani wao wa Simba wanavyochonga juu yao na kuwaambia wawe na akiba ya maneno.

Beki huyo wa kati, aliwatumia salamu mashabiki na viongozi wa Simba akisema hawatakiwi kusema sana juu ya mchezo huo na kwamba, wasubiri matokeo ya uwanjani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dante alisema katika kikosi chao walichopania ni kutwaa taji na sio kuangalia juu ya Simba na kwamba, matokeo ya mchezo huo yatajulikana mwisho wa mchezo.

Alisema amesikia Simba wakisema baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho sasa akili yao ni kuwafunga Yanga na kwamba, hilo halitakuwa jepesi kama wanavyodhani.

Alisema katika mchezo wa kwanza mzunguko wa kwanza ndiyo ulikuwa ukimshtua, lakini baada ya mechi hiyo hakuona kipya katika kikosi cha wekundu hao na mechi ijayo hawatatoka salama.”

“Nimesikia Simba wanasema sasa akili yao ni kwetu ni lazima watufunge, waambieni waweke akiba ya maneno mpira unachezwa uwanjani wasubiri mechi hiyo iishe wapate matokeo,” alisema Dante.

“Simba ni timu nzuri na tunaiheshimu lakini hatuwezi kuanza kupiga kelele sasa, huku kwetu hakuna anayezungumzia mechi hiyo, binafsi niliogopa mechi ile ya kwanza lakini sasa wala sina presha.”

Mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kupigwa Machi 25 kabla ya kupanguliwa na kupelekwa Aprili 6 na kisha kusogezwa mbele kwa siku moja na kutarajiwa ichewe Aprili 7, hatma yake itafahamika leo wakati Bodi ya Ligi itakapotoa ratiba nzima ikiwamo mechi za viporo vya Simba na Yanga. Inaelezwa kuwa mechi hizo za viporo vya Simba na Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar na Njombe Mji zitapangwa kwa kuchezwa kila baada ya siku tatu.