Dante, Ajibu waleta mzuka

Muktasari:

  • Ajibu mwenye mabao saba Ligi Kuu hakuwepo kwenye kikosi kilichocheza mechi mbili za mwisho dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia na Mbeya City kutokana na matatizo ya kifamilia lakini tayari amejiunga na timu na huenda akaanza kwenye mchezo huo wa Jumapili.

MAMBO ya Yanga hapa Morogoro si mchezo unaambiwa, lakini ishu kubwa ni kwamba nyota wake wawili wa kikosi cha kwanza, Ibrahim Ajibu na Andrew Vincent ‘Dante’ tayari wametua kambini kuongeza mzuka siku tatu kabla ya kuwavaa watani zao Simba.

Ajibu mwenye mabao saba Ligi Kuu hakuwepo kwenye kikosi kilichocheza mechi mbili za mwisho dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia na Mbeya City kutokana na matatizo ya kifamilia lakini tayari amejiunga na timu na huenda akaanza kwenye mchezo huo wa Jumapili.

Kurejea kwa Ajibu kunaipa nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo ilikuwa ikimtegemea Obrey Chirwa pekee katika mechi hizo.

Wakati Ajibu akirejesha uhai wa eneo la ushambuliaji, Dante amefufua matumaini ya safu ya ulinzi ya Yanga ambayo ilitikisika kwenye mechi tatu za mwisho alizokosa.

Yanga iliruhusu bao kwenye mechi hizo dhidi ya Dicha, Singida United na Mbeya City ambazo Dante hakucheza jambo ambalo linaonyesha umuhimu wake ndani ya kikosi cha kwanza cha Yanga.

Kurejea kwa Dante huenda kukamrejesha benchi beki Mzanzibari, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye soka lake la kutumia nguvu limezua hofu Yanga kuwa huenda akakumbana na rungu la kadi na kuwagharimu kwenye mchezo huo wa kufa na kupona.

Nyota wengine ambao hawakuwa fiti lakini wanaendelea na mazoezi kuelekea kwenye mechi hiyo ni straika Mrundi, Amissi Tambwe na kiungo Mzimbabwe, Thaban Kamusoko. Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu mara mbili tofauti hajacheza mechi yoyote ya mashindano tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, Kamusoko licha ya kwamba alikuwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Yanga katika mazoezi hayo, alionekana bado hayupo fiti.

ULINZI MKALI

Hali ya ulinzi katika kambi za Simba na Yanga siyo mchezo kabisa. Unaambiwa katika kambi zao mkoani hapa ulinzi umezidi kuimarika tofauti na mechi zao zote ambazo wamekuwa wakiweka kambi.

Simba ambayo ndio ilikuwa ya kwanza kuweka kambi katika mkoa wa Morogoro, waliingia Jumapili na kufanya mazoezi katika Uwanja wa Highland huku wakiweka ulinzi mkali wa kutotaka mazoezi yao kufuatiliwa.

Shabiki mmoja Ally Mohammed mkazi wa Nane nane, alisema alienda uwamjani Highland siku ya Jumatatu lakini alikuta wametanda askari wakikataza mtu asisogee.

“Ilikuwa hatari jamaa hawataki kabisa mazoezi yao yaangaliwe, niliwasha bodaboda mpaka huku nimeambulia patupu bora ningetulia maana mafuta yangu yameemda bure,” alisema.

Yanga nayo iliingia Morogoro Jumatatu na kuhamia katika Uwanja huo huo siku ya Jumanne na kuwafanya Simba wahamie katika Uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.

Makomandoo wa Yanga walikuwa makini kuweka ulinzi wa wachezaji wao kuhakikishwa hata hawaguswi na mashabiki, lakini vile vile walikuwa hawaruhusu watu kuchukua video na walihakikisha hilo kwa kuzunguka mara kwa mara uwanjani hapo.

CHIRWA YUMO

Mashabiki wa Yanga walikuwa na wasiwasi juu ya hatma ya Chirwa baada ya kuzuka taarifa kuwa ana kadi tatu za njano, lakini uongozi wa timu hiyo umesisitiza kwamba mchezaji huyo aliyeifungia Yanga mabao 24 Ligi Kuu Bara tangu ajiunge nayo Juni 2016, atakuwepo katika mchezo huo.

Ziliibuka tetesi kwamba mchezaji huyo ana kadi tatu za njano, lakini uongozi wa Yanga umesisitiza kwamba ana kadi moja ya njano aliyoipata katika mechi ya Mbeya City.

Meneja wa klabu hiyo, Saleh Hafidh alisema; “ Chirwa alikosekana katika mazoezi ya kwanza kutokana na matatizo ya familia, lakini Tshishimbi alikuwa na matibabu, wamemaliza ndio mana wamejiunga hapa,” alisema.