Dah! Samatta ndio basi tena

Muktasari:

  • Katika mchezo huo wa fainali ambao, ulichezwa kwenye Uwanja wa Roi Baudouin mjini Bruxelles, Samatta alianzia benchi na kuingia dakika ya 74 kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis.

NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameshindwa kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa kombe la Ubelgiji, baada ya juzi kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Standard Liège.

Katika mchezo huo wa fainali ambao, ulichezwa kwenye Uwanja wa Roi Baudouin mjini Bruxelles, Samatta alianzia benchi na kuingia dakika ya 74 kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis.

Samatta alionyeshwa kadi ya njano kwenye mchezo huo dakika mbili za ziada kabla ya dakika 90 kumaliza kwa suluhu (0-0) na hatimaye kwenda kwenye dakika 30 za nyongeza ambazo Standard Liège ilijipatia bao.

Fainali hiyo ambayo Genk imepoteza ni fainali ya pili kwa Samatta kupoteza kwenye uchezaji wake wa soka la kimataifa.

Fainali yake ya kwanza alipoteza ni 2013 akiwa na TP Mazembe kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien kwa jumla ya mabao 3-2 huku akifunga mabao sita kwenye mashindano hayo sawa na mfungaji bora, Vincent Die Foneye wa ENPPI Club.

Hata hivyo, 2015, Samatta alishinda fainali yake ya kwanza na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga USM Alger kwa jumla ya mabao 4-1 na akaibuka mfungaji bora kisha akatwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.