Dabno, Christina watamba mbio Bassodawish

Karatu. Mwanariadha Saul Dabno na Christina Faustini wametamba katika mashindano maalumu ya kuibua vipaji vya riadha vya Kids Run vilivyofanyika Kijiji cha Bassodawish Wilaya Karatu.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya wanariadha 219 katika mbio za Km 5 washiriki walikuwa 107, mbio za Km 2.5 wakiwa 112.

Katika mbio za km 5, Saul Dabno alishinda akitumia dakika 13:03, akifutwa na Emmanuel Paulo aliyetumia dakia 13:05, nafasi ya tatu ikienda kwa Elibariki Martin aliyetumia dakia 13:09, Modest Marcel akimaliza nafasi ya nne na Joel Tango akimaliza nafasi ya tano kwa kutumia muda wa dakika 13:13.

 Kwa wanawake Christina Faustini alimaliza kidedea akitumia dakia 15: 01, akifuatwa na Monica Muhuri aliyetumia dakika 15:03, Maria Daniel alimaliza nafasi ya tatu kwa kutumia dakika 16:06 na nafasi ya nne ikienda kwa Juliana Mosses akitumia dakika 16:10.

Kwa watoto waliokimbia Km 2.5, Anthon Pascal alimaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 7:25, Benardo Gabriel akishika nafasi ya pili akitumia dakika 7:27 na Joshua Paulo akimaliza nafasi ya tatu baada ya kutumia dakika 7:30.

Kwa wasichana Maria Wilfred alimaliza wa kwanza akitumia dakika 8:03, Juliana Oldian alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 8: 10 na Rosemary John akimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 8:16.